Makamu wa Rais , Samia Suluhu Hassan anaondoka nchini leo kwenda London, Uingereza kushiriki
kwenye Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaotarajiwa
kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 20 Aprili, mwaka huu akimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli.
Mkutano huo ambao Kaulimbiu yake ni “Kuelekea
Mustakabali wa Pamoja” utafanyika chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Uingereza,
Mheshimiwa Theresa May na utafunguliwa na Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Malkia
Elizabeth wa Pili wa Uingereza.
Majadiliano ya Mkutano wa CHOGM 2018 yatajikita kwenye
maeneo manne makuu ya kipaumbele ambayo yatajadili namna Jumuiya ya Madola inaweza
kufikia mustakabali wenye ustawi zaidi; mustakabali endelevu zaidi; mustakabali
wenye haki zaidi; na mustakabali wenye usawa zaidi.
Mijadala katika maeneo hayo ya kipaumbele itahusisha
masuala mbalimbali ikiwemo, kukuza zaidi biashara na uwekezaji baina ya nchi za
Jumuiya ya Madola kwa manufaa ya nchi wanachama na Jumuiya nzima; kukuza na kuendeleza
misingi ya demokrasia; ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo endelevu
pamoja na masuala ya uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uhalifu wa kimtandao
na usafirishaji wa binadamu.
Jumuiya ya Madola ilianzishwa mwaka 1949 kupitia Tamko
la London ambalo lilikuwa ni matokeo ya Mkutano wa Mawaziri Wakuu wa Nchi za
Jumuiya ya Madola. Jumuiya ya Madola ina
wanachama 53 ambapo kati ya hizo, nchi 19 ni za Afrika, 7 ni kutoka Asia, 13 ni
kutoka nchi za Carribean na Mabara ya Amerika, 11 ni kutoka eneo la Pacific na nchi
3 ni kutoka Ulaya.
Ujumbe wa Makamu wa Rais unajumuisha, Dkt.
Balozi Augustine Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirkiano wa Afrika Mashariki.
Makamu wa Rais na ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini
Aprili 22, mwaka huu.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment