Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo yenye dhamana ya kusimamia Maendeleo ya
sekta ya filamu nchini, inatoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa
Dar-es-salaam, Paul Makonda, kwa kuunga mkono jitihada za Wizara za kuendesha operesheni dhidi ya kazi haramu za filamu, kazi ziziso na maadili pamoja nakuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaouza kazi hizo.
Dhamira ya
Mkuu wa Mkoa inalenga ulinzi wa jamii dhidi ya kazi chafu na pia kutetea maslahi
na haki za wadau wa tasnia ya filamu.
Wizara pia
inaunga mkono tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuzipiga marufuku filamu
za utupu na kuwachukulia hatua wanaoziuza,sambaza na wanazionesha filamu za
aina hiyo kwenye vibanda visivyo rasmi. Hatua hizi za Mkuu wa Mkoa ni
utekelezaji wa Sheria mbalimbali za nchi ikiwemo Sheria yenye kusimamia Filamu
na ile ya hakimiliki na hakishiriki.
Wizara
itashirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama
katika kuhakikisha dhamira hii njema inatekelezwa na inakuwa endelevu kwa
kuhusisha nchi nzima; na inatoa wito kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini kuunga
mkono jitihada hizi za Serikali katika maeneo yao.
Wizara
inapenda kuwahakikishia watanzania kwamba ni haki ya msingi kupata burudani
stahiki katika maeneo yao kupitia mifumo mbalimbali ya usambazaji wa kazi za
filamu hata hivyo haitawavumilia wale wote wanaoendesha shughuli hizo kinyume cha
sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Aidha, inatoa rai kwa wafanya biashara,wadau
wa filamu na umma kwa ujumla kuzingatia Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza
na Kanuni zake, Kanuni za Stempu kwa
bidhaa za Filamu na Muziki za mwaka 2013 kabla ya kuingiza nchini, kuzalisha,
kuonyesha na kuzipeleka kwa walaji kupitia njia yoyote ya kusambaza kazi hizo.
“Filamu
ni uchumi Filamu ni ajira, tutumie filamu kuchochea maendeleo endelevu”
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment