Rais
Dkt.John Pombe Magufuli akiagana na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Daniel
Fred Kidega mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
**************
Spika
wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Daniel Kidega amempongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ya kujenga
uchumi wa Tanzania na amewaomba wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki kuunga
mkono mfano mzuri unaooneshwa na kiongozi huyo.
Mhe.
Daniel Kidega amesema hayo leo Februari 13, 2017 Ikulu Jijini Dar es
Salaam muda mfupi baada ya kukutana na Mhe. Rais Magufuli na kufanya nae
mazungumzo yaliyojikita kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya
nchi wanachama, kuinua hali ya uchumi na kutatua matatizo yanayozikabili baadhi
ya nchi wanachama wa Jumuiya.
“Nikueleze
kitu kimoja, Tanzania na Afrika Mashariki tumebahatika sana kupata kiongozi
kama Rais Magufuli ambaye anatuongoza vizuri, analeta maendeleo na mabadiliko,
naomba watu wote wa Tanzania na Afrika Mashariki wamuunge mkono, kwamba
kiongozi kama yeye ndiye tunayemtaka, tuangalie viongozi wanaoleta maendeleo na
mabadiliko kwa watu wetu ili tuwe vizuri”
amesisitiza Mhe. Daniel Kidega.
Wakati huo huo,
Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza hapa
nchini Mhe. Sarah Cooke ambapo viongozi hao wamezungumzia namna Tanzania na
Uingereza zitakavyoimarisha uhusiano na ushirikiano katika uwekezaji na
biashara, mapambano dhidi ya Rushwa na dawa za kulevya, kuimarisha ukusanyaji
wa mapato ya Serikali na kuimarisha huduma za usafiri wa anga.
Kwa
upande wake Mhe. Dkt. Magufuli amemshukuru Mhe. Sarah Cooke na kumhakikishia
kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na uhusiano wake wa
kihistoria na Uingereza katika kujenga uchumi imara wa Tanzania, kupambana na
rushwa na dawa za kulevya na amemshukuru Uingereza kuongeza fedha katika
utekelezaji wa miradi mbalimbali itakayosaidia maendeleo hapa nchini.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi Mpya wa
Shirika la Fedha Duniani (IMF) Bw. Bhaswar Mukhopadhyay ambapo viongozi hao
wamezungumzia juu ya shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa kwa
ushirikiano wa Tanzania na IMF.
Bw.
Bhaswar Mukhopadhyay amempongeza Rais Magufuli kwa hatua kubwa na muhimu
anazochukua kuimarisha uchumi, zilizowezesha kiwango kizuri cha ukuaji wa
uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa.
Halikadhalika
Mhe. Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Mhe. Balozi
Liberat Mfumukeko.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment