Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Nafasi Ya Matangazo

Thursday, 22 June 2017

RAIS MAGUFULI AMALIZA ZIARA YA SIKU 3 PWANI ATOA MAAGIZO

Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo Juni 22, 2017 amemaliza ziara yake ya siku 3 Mkoani Pwani kwa kumuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage kuwanyang’anya viwanda watu wote waliouziwa viwanda na Serikali na baadaye kuvitelekeza ili wapatiwe wawekezaji wengine wanaoweza kuviendeleza.

Rais Magufuli amesema kuna viwanda 197 ambavyo viliuzwa kwa watu mbalimbali kwa lengo la kuviendeleza lakini viwanda hivyo vimekufa na vingine kubadilishiwa matumizi jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi za kutekeleza mpango wa ujenzi wa viwanda.

“Waziri wale waliopewa viwanda miaka ile kwa kuuziwa bei ya chee, tukitegemea kwamba vile viwanda vitaendelea kufanya kazi lakini wamevitelekeza na vingine havipo kabisa, usiwe na kigugumizi na wala usiangalie sura, wanyang’anye, wale wawekezaji wenye nia ya kujenga viwanda wapewe, kiwanda sio mwanamwali wa kumtunza ndani, kinatakiwa kifanye kazi kitoe ajira na Serikali ipate mapato” amesema  Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kusindika matunda cha Sayona Fruits Ltd kilichopo katika Kijiji cha Mboga Wilayani Chalinze ambacho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kusindika tani 300 za matunda kwa siku, kuajiri wafanyakazi 800 na kitawanufaisha wakulima 30,000.

Kiwanda hicho kinajengwa na Mtanzania Subhash Patel kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 120.
Kabla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho, Rais Magufuli ametembelea kiwanda cha kutengeneza dawa za viuadudu cha Kibaha ambacho kimejengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Cuba kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 22.3 kwa lengo la kuzalisha dawa za kuangamiza viluilui vya mbu na kutokemeza ugonjwa wa malaria.

Akiwa kiwandani hapo Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa Shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya kununulia lita takribani 100,000 za viuadudu zilizokwama kiwandani hapo kutokana na Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kutozinunua na ameelekeza kuwa halmashauri zote zitakazopangwa kuchukua viuadudu hivyo ziwe zimechukua kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Julai.

“Hatuwezi kuwa tunaanzisha viwanda kama hiki cha dawa halafu hatuvitumii, kinazalisha dawa wanatumia watu wa nchi zingine wakati sisi tunaendelea kufa kwa malaria” amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amezindua barabara ya Bagamoyo – Makofia – Msata yenye urefu wa Kilometa 64 na kuipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na wote waliofanikisha ujenzi wa barabara hiyo ambayo inasaidia kutatua tatizo la msongamano wa magari katika barabara ya Chalinze – Dar es Salaam na inapita katika eneo la Bagamoyo ambalo litajengwa bandari mpya na eneo la viwanda.

Ujenzi wa barabara hiyo yenye madaraja makubwa matatu umegharimu Shilingi Bilioni 213 ikiwa ni fedha zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Rais Magufuli pia amezindua kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agri Company Ltd kilichopo katika kijiji cha Mapinga Wilayani Bagamoyo ambacho kina uwezo wa kukausha tani 60,000 za matunda kwa mwaka na kimewekezwa na mwekezaji Mtanzania kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 26.4

Akiwa kiwandani hapo, Rais Magufuli amesema Serikali yake haitatoa fidia kwa watu ambao wanadai kulipwa fidia kutokana na maeneo yao kuchukuliwa ili kupisha mradi wa ujenzi wa eneo la bandari na viwanda la Bagamoyo na ameagiza watu waliofanya njama za kulipwa fidia wakati hawakustahili fidia hizo warudishe fedha mara moja kabla hatua za kisheria hazijaanza kuchukuliwa dhidi yao.

Wakati huo huo,  Rais Magufuli amesema Serikali yake haitaruhusu wanafunzi wa shule za msingi na sekondari watakaopata ujauzito kuendelea na masomo.

Rais Magufuli amesema Serikali ina wajibu wa kulinda misingi ya kitaifa na kusimamia mienendo ya wanafunzi wawapo shuleni na amesisitiza kuwa kuwaruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo kutasababisha wanafunzi wengi kujihusisha na vitendo vya mapenzi shuleni.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment