WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kwa wafanyabiashara na wenye
viwanda vya mafuta ya kupikia na sukari nchini kuhakikisha bidhaa hizo
zinaendelea kupatikana katika maeneo yote na katika bei ya kawaida.
“Natoa
siku tatu kuanzia kesho Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi mafuta yote
yaliyoko bohari yaondolewe yaendelee kusambazwa kama kawaida nchini kote
ili kuondoa uhaba uliojitokeza na kamwe Serikali haitokubali kuchezewa na wafanyabiashara wasiowaaminifu,”
Ametoa
agizo hilo leo jioni (Jumatano, Mei 9, 2018) Bungeni Jijini Dodoma mara
baada ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage
kutoa kauli ya Serikali kuhusu uhaba wa mafuta ya kupikia nchini.
Amesema
kama uhaba wa bidhaa hiyo utaendelea, ifikapo Jumapili Serikali itaanza
kufanya msako kwenye viwanda na maghala na kuchukua hatua kali kwa
watakaobainika kuficha mafuta hayo.
Waziri
Mkuu amesema takwimu zinathibitisha kwamba mafuta ya kupikia
yaliyoingizwa nchini yanatosha, hivyo nchi haipaswi kuwa na uhaba.
Amesema kwa mwezi mafuta yanayotumika nchini tani 28.9 na kila mwezi
zinaingizwa tani 30,000.
“Hatuwezi
kukubaliana na jambo hili kwa sababu haliko kwa bahati mbaya ni mpango
uliopangwa kwani imekuwa ni kawaida kila tunapoelekea kwenye Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani kunakuwa na upungufu wa bidhaa hasa sukari, hivyo
Serikali haitakubali wananchi wateseke bila sababu za msingi,”
amesisitiza.
Akiwasilisha kauli ya Serikali Bungeni,
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mwijage alisema vyanzo
vinavyotumika kuzalishia mafuta nchini vinatosheleza mahitaji kwa
asilimia 30, hivyo asilimia 70 ya mafuta huagizwa kutoka nje ya nchi.
“Miezi
mitatu ya mwanzo kwa mwaka huu kuanzia Januari wastani wa mafuta
yaliyoingizwa ni tani 30,210.71 kwa mwezi na jumla ya akiba ya mafuta
yaliyopo nchini ni wastani wa tani 68, 902, hivyo hakuna upungufu,”
alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment