Makamu wa
Rais , Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuzindua mradi
mkubwa wa maji Vijijini ambao umegharimu
zaidi ya shilingi bilioni 28 na utahudumia wananchi 42,000 katika wilaya SABA
za mkoa wa TABORA.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amezindua mradi
mkubwa wa maji Vijijini ambao umegharimu
zaidi ya shilingi bilioni 28 na utahudumia wananchi 42,000 katika wilaya SABA
za mkoa wa TABORA.
Uzinduzi wa
mradi huo mkubwa na wa aina yake katika mkoa wa Tabora umetekelezwa na Serikali
ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (JICA) kwa ushirikiano
na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza
katika halfa ya Uzinduzi wa Mradi huo katika Kijiji cha Mabama wilaya ya Uyui
mkoani Tabora, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia
Suluhu Hassan amesema kuwa nia ya Serikali ni kuona wananchi wa mkoa wa Tabora
wanapata maji safi na salama karibu na maeneo yao kama hatua ya kukomesha
tatizo sugu la maji kwa wananchi wa mkoa huo.
Makamu wa
Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa
kuhakikisha wananchi kote nchini wanapata maji safi na salama kwa muda wote
hivyo jitihada mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha tatizo sugu
la maji safi la salama katika baadhi ya maeneo nchini linapata ufumbuzi wa
kudumu.
Kuhusu
utekelezaji duni wa baadhi ya miradi ya maji nchini, Makamu wa Rais ameonya
kuwa Serikali kamwe haitawavumilia watumishi au wakandarasi ambao watatekeleza
miradi ya maji ya wananchi kwa kiwango hafifu na watakaobainika watachukuliwa
hatua kali za kisheria.
Amesema kuwa
Serikali kwa ushirikiano na wahisani mbalimbali wamekuwa wakitoa fedha nyingi
za miradi ya maendeleo hasa miradi ya maji lakini kumekuwepo na tabia ya baadhi
wa watendaji wa Serikali kutumia vibaya fedha hizo na kusema kuwa muda wa
watendaji hao kuiba fedha hizo umeshaisha na watakaobainika kufanya hivyo
watawajibishwa ipasavyo ili kuwa fundisho kwa watu wengine.
Aidha,
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pia amewahimiza wananchi wa mkoa wa Tabora
kuutunza ipasavyo mradi huo ili uweze kuwanufaisha kwa muda mrefu wananchi wote
wa mkoa huo.
Katika
Hotuba yake Makamu wa Rais amewataka Viongozi wa mkoa wa Tabora kupambana ipasavyo
na watu wanaoharibu mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji kama hatua ya
kuhakikisha maeneo yanahifadhiwa.
Kwa upande
wake, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo wa
Maji Vijijini utahudumia vijiji 31 katika wilaya Saba za mkoa wa Tabora.
Waziri
Lwenge ameeleza kuwa mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa
Tabora kwa sababu mkoa huo ni moja ya mikoa kadhaa hapa inayokabiliwa na ukame
mkubwa.
Amesema kuwa
Serikali ya awamu ya Tano itaendeleo kuweka mipango na mikakati mizuri
inayolenga kuhakikisha wananchi nchini wanapata maji safi na salama ili
kuboresha maisha yao na kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande
wake, Balozi wa Japan hapa nchini Masaharu Yoshida amesema kuwa Serikali ya
Japan imetekeleza mradi huo maji ambao utanufaisha maelfu ya wananchi wa Tabora
kutokana na mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Japan.
Balozi Masaharu
Yoshida amesema kuwa upatikanaji wa maji ni jambo la msingi na muhimu kwa ajili
ya usalama wa binadamu na utasaidia wananchi katika shughuli za uzalishaji
badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.
Balozi huyo pia
ameahidi Serikali ya Japan itaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa Tanzania
kufutana na matakwa ya Serikali kwa ajili ya kuboresha hali ya maisha na ustawi
wa taifa na wananchi kwa ujumla.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment