Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa
akiangalia Mtoto wa Darasa la asaba Uhuru Mchanganyiko Mariana Alex
Mwenye ulemavu wa macho
, anavyo weza kuandika
kwakutumia mashine maalumu
ya kuandika , June 6 2017
Waziri Mkuu alikabidhi
vifaa vya Kujifunzia katika
shule mbali mbali hapa Nchini Shughuli hiyo imefanyika Jijini
Dar es salaam
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akijaribu
kuandika kwakutumia kifaa maalumu
chakujifunzia kuandika watoto wenyeulemavu wa
Macho 6 june2017, Kulia kwa
Waziri Mkuu ni Waziri wa Elimu na Sayansi
Profesa Joyce Ndalichako,
Waziri Mkuu alikabidhi
vifaa vya Kujifunzia katika shule mbali mbali hapa Nchini
Shughuli hiyo imefanyika Jijini Dar es salaam
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi wote
nchini ambao wana watoto wenye ulemavu wasiwafiche na badala yake wahakikishe
wanapata elimu na kutimiza ndoto zao.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumanne, Juni 6,
2017) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, walimu na
wanafunzi kwenye uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya elimu maalum uliofanyika
kwenye viwanja vya ya msingi Uhuru Mchanganyiko, jijini Dar es Salaam.
“Nikiwa mwalimu kitaaluma, natambua kwamba
mapungufu ya kimwili, kisaikolojia, kiakili au ulemavu wa aina yoyote si
kikwazo cha kutimiza ndoto za watoto wetu. Hili linadhihirika kwenye maeneo
mbalimbali nchini,” alisema na kutoa mfano wa utumishi Serikalini ambako kuna
viongozi wenye mahitaji maalum, lakini wamekuwa wakitoa mchango mkubwa bila
kujali hali yao kimwili au vinginevyo.
“Hivyo,
nawasihi wazazi wenzangu, msikatishe ndoto za watoto wenu wenye mahitaji maalum
kwa kuwaficha. Wapelekeni shuleni wakapate elimu, iwafae maishani,” alisema.
Waziri Mkuu alisema usambazaji wa
vifaa hivyo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya
kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania mwenye umri wa kwenda shule, anapata
huduma hiyo bila kujali hali yake ya kimwili, kiakili, kiafya na uwezo wa
kifedha.
Waziri Mkuu pia alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi
Rais (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene ahakikishe anandaa utaratibu wa
kuwatambua watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kupangiwa bajeti kulingana
na mahitaji yatakayoainishwa.
“Tunapoendelea na jitihada hizi za
kuwawezesha watoto wenye mahitaji maalum kupata elimu, ni vizuri tukawa na
utaratibu endelevu wa kubaini idadi kamili ya watoto hao kupitia uandikishaji
wa watoto shuleni. Bila kubaini idadi yao, itatuwia vigumu kupanga bajeti kwa
ajili ya watoto wetu hao. Zoezi hili linaweza kufanyika wakati wa uandikishaji
na likawa endelevu kadiri wanavyopanda vidato,” alisema.
Waziri Mkuu alisema mbali ya vifaa
vya wanafunzi wasioona na wenye baki ya usikivu (hard of hearing), Serikali pia
imenunua vifaa kwa ajili ya walimu wao ili vitumike kufundishia na kupimia ili
kubaini mahitaji maalum ya ujifunzaji kwa watoto wanaoandikishwa shuleni.
Alisema
vifaa vinavyoanza kusambazwa, vitasaidia kuinua kiwango cha taaluma kwenye
shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum na pia vitasaidia watoto wengi
zaidi wenye mahitaji maalum wapate elimu na kuongeza hamasa kwa walimu
wanaofundisha kwenye shule husika.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia hadhira hiyo, Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alisema uzinduzi wa zoezi la
usambazaji wa vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa utahusisha
mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kwamba zoezi hilo litazinufaisha shule za
msingi 213 kati ya 408; na shule za sekondari 22 kati ya 43 zenye wanafunzi wa mahitaji maalum.
Alisema vifaa vilivyonunuliwa
vimegharimu sh. bilioni 3.6 kutokana na michango ya
washirika wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia, Shirika la Misaada ya Maendeleo
ya Kimataifa (DfID) na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Sweden (SIDA) na kwamba wizara hiyo itaendelea
kununua vifaa zaidi kulingana na bajeti inayotolewa.
Alivitaja vifaa vilivyoninunuliwa
kuwa ni mashine za nukta nundu 932; vivunge vya kufundishia wasioona 1,495; karatasi
za kuandikia nukta nundu (ream) 2,548; karatasi za kurudufishia (ream) 1,150;
shime sikio (hearing aid) 1,150 na vivunge vya upimaji wa mahitaji maalum ya
kielimu 78.
Naye Mratibu wa Elimu kutoka SIDA, Bi. Helena
Reutersward akitoa salamu kwa niaba ya washirika wa maendeleo alisema wao
wamedhamiria kuboresha sekta ya elimu hapa nchini na hasa elimu kwa watoto
wenye mahitaji maalum.
“Elimu ni muhimu ni kwa kila mtu lakini ni muhimu
zaidi kwa watu wenye mahitaji maalum. Washirika wa maendeleo tutaendelea
kushirikiana na Serikali katika kuchangia jitihada zake za kuboresha elimu
nchini Tanzania,” alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment