MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema kamwe Serikali haitagawa
chakula kwa wananchi wavivu ambao hawataki kufanya kazi na kusubiri chakula
kutoka Serikalini.
Makamu wa Rais, Samia ametoa kauli hiyo wakati
akihutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Musoma katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye uwanja wa Mukendo mjini Musoma.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali itapeleka chakula kwa wananchi ambao
mazao yao yaliharibiwa kwa mvua au yalikauka kwa ukame au kwa maafa
mengine na sio kwa wananchi wanaokaa vijiweni mchana kutwa bila kufanya kazi
wakisubiri neema ya chakula kutoka kwa Serikali.
Amewahimiza wananchi kote
nchini kuendelea kufanya kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo na pindi
wanapovuka wajiwekee akiba na waache tabia ya kuuza mazao yote wanayovuka ili
kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula kwenye familia zao.
Makamu wa Rais pia amewataka
viongozi wa mkoa wa Mara washirikiane na wananchi katika kuwaelemisha mbinu
bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi ikilinganishwa na hali ilivyo kwa
sasa.
Kuhusu tatizo la uvuvi haramu,
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan
ameziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama kufanya misako ya hali na mali katika
kupambana na tatizo hilo ambalo limechangia kupunguza samaki katika maeneo
mbalimbali nchini.
Ametoa mfano kwa mkoa wa Mara
kuwa ulikuwa na viwanda Vinne vya kuchakata samaki lakini kutokana na shughuli
za uvuvi haramu na wa kutumia sumu umepelekea viwanda Vitatu kukosa malighafi
hiyo na kusitisha uzalishaji.
Makamu wa Rais amesema jambo hilo ni baya kwa sababu limeikosesha Serikali
mapato na kusababisha wananchi wakose ajira kutoka kwenye viwanda hivyo
jitihada za makusudi lazima zifanyike katika kukomesha uvuvi haramu katika
maeneo mbalimbali nchini hasa katika Ziwa Victoria.
Aidha, Makamu wa Rais ameeleza
kufurahishwa na kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Musoma ambao umetekelezwa
na Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ufaransa na kusema kuwa mradi huo
utaondoa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa wilaya ya
Musoma.
Amewataka wananchi wa Manispaa
ya Musoma kuulinda na kuutunza mradi huo ili uweze kudumu kwa miaka mingi kwa
ajili ya kuhudumia wananchi wa Manispaa hiyo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara
Dakta Charles Mlingwa amewahimiza wananchi wa mkoa wa Mara kuweka itikadi zao
kando na washirikiane katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo
mkoani humo.
Nilistaajabu nilipomuona bibi kizee akilima peke yake licha ya kuwa na watoto pamoja na wajukuu ambao huonekana wakilandalanda mtaani.
ReplyDeleteBy:Mawazo Mwangobola