Na Beatrice
Lyimo-MAELEZO
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa hatua kali
zitachukuliwa kwa atakayepokea rushwa kutoka kwa wauzaji, wasambazaji na
watumiaji wa Madawa ya Kulevya.
Ameyasema hayo leo jijini
Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza cha Baraza la Taifa la
kudhibiti dawa za kulevya nchini.
“Sheria ya udhibiti
wa madawa ya kulevya itumike vizuri, Serikali na Baraza halitahitaji mtu yeyote
mwenye mamlaka kupokea rushwa ikigundulika hatua kali zitachukuliwa” alifafanua
Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu
alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuendelea kuimarisha
mapambano dhidi ya udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini ambayo yamekuwa
yakifanywa na Serikali za Awamu zilizotangulia.
Aidha, Waziri Mkuu alisema
kuwa mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya ni vita inayotakiwa kupigana kwa nguvu
kubwa kwani madhara ya dawa hizo ni kubwa kwa jamii hususani vijana ambao ni
nguvu kazi ya taifa.
“Tunahitaji
ushirikiano wa karibu wa pande zote mbili za Muungano kwani tatizo hili limeathiri
pande zote na ukanda wa bahari unatumika sana kama njia ya kuingiza dawa hizo”
“Wakuu wa Mikoa mna
kazi kubwa katika vita hii, mkiwa wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama mpo
kwenye nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na
Taratibu zilizopo” alisema Waziri Mkuu.
Hata hivyo Waziri
Mkuu alibainisha kuwa, wajibu wa Baraza ni kusimamia utekelezaji wa Sera ya
Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, ambapo jukumu hilo ni kubwa na wajumbe wa
Baraza hilo wanatakiwa kulitekeleza kwa uadilifu na umahiri mkubwa.
Baraza la Taifa la
kudhibiti Dawa za Kulevya limeanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 ambapo Waziri
Mkuu ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo pamoja na wajumbe wengine wakiwemo Waziri
anayeshughulikia Mambo ya Sheria, Waziri anayeshughulikia Mambo ya Ndani ya
Nchi.
Wengine ni Waziri
anayeshughulikia Afya, waziri anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Waziri
anayeshughulikia Mambo ya Nchi za Nje, Waziri anayeshughulikia Fedha, Waziri
anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Waziri anayeshughulikia Elimu, Waziri
anayeshughulikia Kilimo, Waziri anayeshughulikia Uchukuzi na Waziri anayeshughulikia
Ulinzi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment