WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waulinde
Muungano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar na akawaonya wasitumie Bunge hilo kuupotosha.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 10, 2018) Bungeni mjini Dodoma kwenye mkutano
wa 11 wa Bunge, wakati akihitimisha mjadala wa mapitio ya utekelezaji wa kazi
za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka
2018/2019.
Waziri
Mkuu amesema mjadala ulioibuka jana kuhusu suala la Muungano haukuwa na afya na
kwamba hatarajii kuona hali hiyo ikijirudia tena Bungeni kuhusiana na suala la
Muungano.
“Mjadala
wa jana sijaupenda kabisa na wala haukuwa na afya, ulikuwa ni malumbano baina
waheshimiwa wabunge wawili. Hatuzuii Mhe. Mbunge kuuliza jambo ili apate
ufafanuzi lakini pia haturuhusu mtu na mtu watumie Bunge kupotosha ukweli wa
mambo,” alisisitiza.
Waziri Mkuu amelieleza Bunge
kwamba kuna maboresho ambayo yanafanywa hivi sasa na Serikali za pande zote
mbili lakini akatumia fursa hiyo kulihakikishia Bunge kwamba majadiliano bado
yanaendelea kwenye vikao halali vya SMT na SMZ ambavyo vinaongozwa na Makamu wa
Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akitoa ufafanuzi kuhusu chanzo
cha malumbano hayo, Waziri Mkuu alisema kiini cha malumbano hayo ni suala la uagizaji
sukari kutoka nje ya nchi ili kufidia upungufu wa sukari uliopo nchini (gap
sugar). Alisema katika kutimiza azma hiyo, Serikali haiangalii kama muagizaji
ametoka Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu
alisema katika mwaka 2016, upungufu uliojitokeza ulikuwa tani 140,000 lakini
waagizaji waliopewa vibali walikuwa wawili kutoka Zanzibar, watatu kutoka Bara
na kiwanda cha sukari cha Mahonda kilipewa kibali cha kuagiza tani 390.
“Katika mwaka 2017, gap
sugar ilikuwa tani 140,000 na waliopewa vibali walikuwa ni wawili kutoka
Zanzibar na wawili kutoka Bara, lakini kwa mwaka huu (2018) gap sugar ni tani
135,000. Tofauti na miaka ya nyuma, safari hii tumewapa vibali wenye viwanda
ndiyo waagize sukari kutoka nje. Kwa hiyo, jambo hili la sukari lisivuruge
Muungano wetu,” alisisitiza.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment