Jengo la ghorofa 12 la PSPF DODOMA PLAZA
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 23
Aprili, 2018 amefungua jengo la mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSPF, ofisi ya
makao makuu ya benki ya NMB Mjini Dodoma na matawi mawili ya benki hiyo.
Jengo
la PSPF lenye ghorofa 11 lina ukubwa wa mita za mraba 15,741.60, limejengwa kwa
gharama ya Shilingi Bilioni 30.56 na ndani ya jengo hilo ndimo benki ya NMB
imefungua ofisi zake za makao makuu, tawi la benki kwa wateja maalum, na tawi
la benki kwa wateja binafsi lililopewa jina la Kambarage kwa lengo la kumuenzi
Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Mkurugenzi
Mkuu wa PSPF Bw. Adam Mayingu amesema jengo hilo ambalo tayari limeshapata
wapangaji kwa asilimia 98 wengi wao wakiwa ofisi za umma, linatarajiwa
kuzalisha Shilingi Bilioni 4.7 kila mwaka na litarejesha fedha za uwekezaji
ndani ya miaka 8 na kwamba katika juhudi hizo hizo za kuunga mkono Serikali
kuhamia Dodoma PSPF inatekeleza mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba 500 kwa
ushirikiano na mfuko wa hifadhi ya jamii wa Watumishi Housing.
Mkurugenzi
Mtendaji wa benki ya NMB Bi. Ineke Bussemaker amesema benki hiyo yenye matawi
218 ndio benki kubwa inayoendeshwa kwa faida hapa nchini na ikiwa na kiwango
kidogo cha mikopo chechefu, imekuwa ikichangia katika bajeti ya nchini kupitia
kodi na gawio ambapo katika miaka mitatu iliyopita imechangia Shilingi Bilioni
16.525 kila mwaka na katika sherehe hizo amechangia Shilingi Milioni 50 kwa
maendeleo ya Dodoma.
Akizungumza
kwa niaba ya Mke wa Baba wa Taifa Mhe. Mama Maria Nyerere, Mtoto wa Baba wa
Taifa Bw. Makongoro Nyerere ameishukuru benki ya NMB kwa kutambua mchango wa
Baba wa Taifa na kuamua tawi hilo liitwe jina lake la “Kambarage”
na pia ametoa wito kwa vijana kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais
Magufuli.
“Mhe. Rais
wewe chapa kazi, hawa wanaokushambulia hata wakati wa Baba wa Taifa walikuwepo
na wengine walikimbilia nchi nyingine, wewe chapa kazi”
amesisitiza Bw. Makongoro Nyerere.
Akihutubia
kabla ya kufungua rasmi miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza PSPF kwa
kuwekeza katika jengo ambalo tayari limeshapata wapangaji na pia ameipongeza
mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuitikia wito wa kuwekeza katika viwanda 16
ambavyo vitazalisha ajira na kuchangia katika uchumi wa nchi.
Mhe.
Rais Magufuli pia ameipongeza benki ya NMB kwa kazi nzuri inayofanya na kwa kuwafikishia
huduma Watanzania wengi, lakini ametaka katika mwaka huu wa 2017/18 benki hiyo inayomilikiwa
na Serikali kwa asilimia 32 iongeze gawio.
“Mwaka
2012/13 Benki ya NMB ilitoa gawio kwa Serikali la Shilingi Bilioni 10.805,
mwaka 2013/14 ikatoa Shilingi Bilioni 14.301, mwaka 2014/15 ikatoa Shilingi
Biliongi 16.525, mwaka 2015/16 ikatoa gawio hilohilo la Shilingi Bilioni 16.525
na mwaka 2016/17 ikatoa tena gawio hilohilo la Shilingi Bilioni 16.525, yaani
miaka mitatu mfurulizo mnatoa gawio lilelile wakati mnatuambia faida ya benki
imekua, nataka mnaoiwakilisha Serikali kwenye NMB mkaliangalie hili na gawio la
mwaka 2017/18 liongezeke” amesema Mhe. Rais
Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amejibu ombi lililotolewa na Mbunge wa Dodoma Mjini Mhe.
Anthony Mavunde la kupunguzwa kwa tozo ya kodi katika mchuzi wa zabibu, na
amewataka wadau wanaohusika wakiwemo wabunge kufanyia kazi ombi hilo kwa zao la
zabibu na mazao mengine ya kilimo na mifugo hapa nchini ili tozo za kodi
zisisababishe bidhaa za wazalishaji wa Tanzania kushindwa kushindana na bidhaa
zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi.
Mhe.
Rais Magufuli pia amemshukuru Mtoto wa Baba wa Taifa Bw. Makongoro Nyerere kwa
ujumbe wake kwa Watanzania hasa vijana na amemhakikishia kuwa Serikali anayoiongoza
ipo imara na itaendelea kuwa imara kusimamia misingi ya kulijenga Taifa.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment