Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Rais wa Kenya
Uhuru Kenyatta mara baada ya kupiga picha ya pamoja na Mawaziri pande zote
mbili za Kenya na Tanzania mara baada ya kikao chao Kampala nchini Uganda.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kabla ya mazungumzo yao jijini Kampala.
Rais Dk John Magufuli mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa
Tanzania, Benjamin William Mkapa ambaye ni mratibu wa mazungumzo ya
amani ya mgogoro wa Burundi
Rais
Dkt. John Magufuli na Rais wa Uhuru Kenyatta wamewaagiza
Mawaziri wa Tanzania na Kenya kutatua tofauti ndogondogo zinazojitokeza
katika biashara kati ya nchi hizi mbili.
Marais
hao wametoa maagizo hayo leo asubuhi tarehe 23 Februari, 2018
walipokutana na kufanya mazungumzo katika hoteli ya Munyonyo mjini
Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa
nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais
Magufuli na Rais Kenyatta wamesema wanataka kuona biashara kati ya
Tanzania na Kenya inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina
ya nchi hizo bila vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti
zilizojitokeza katika baadhi ya bidhaa zimalizwe.
“Kuna
mambo madogomadogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya
na Tanzania, tunataka kwa haya yote Mawaziri wa Kenya na Mawaziri wa
Tanzania mkae myatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogomadogo
mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa
myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa” amesema Mhe.
Rais Magufuli na kuungwa mkono na Mhe. Rais Kenyatta.
Wametoa
maagizo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki wa Tanzania Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria
wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya
Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya
Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya, Peter Munya.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa
Jamhuri ya Sudani Kusini, Salva Kiir Mayardit katika hoteli ya Munyonyo
Mjini Kampala.
Baada
ya Mazungumzo hayo, Rais Magufuli amesema Tanzania kama ilivyo kwa
nchi nyingine za Afrika Mashariki inaguswa na hali ya Sudani kusini na
ametoa wito kwa pande zinazopingana kumaliza tofauti zao ili wananchi wa
Sudani Kusini wajikite kujenga nchi yao.
“Nimemhakikishia
Rais Salva Kiir kuwa Tanzania ipo pamoja na Sudani Kusini na
tunapenda tofauti zinazosababisha matatizo nchini mwake ziishe, sisi
Tanzania tupo tayari kufanya biashara na Sudani Kusini, hata chakula
kama wanahitaji tutawauzia” amesema, Rais Magufuli.
Kwa
upande wake, Rais Salva Kiir Mayardit amesema Tanzania na Sudani Kusini
zina uhusiano wa kihistoria tangu enzi ya Baba wa Taifa Hayati Mwl.
Julius Kambarage Nyerere na kwamba japo kuna vita nchini mwake, Rais
Magufuli amemhakikishia kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaendelezwa na
kukuzwa zaidi.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Gaston Sindimwo.
Gaston
Sindimwo amemfikishia ujumbe wa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuwa
hali ya Burundi ni shwari na Mhe. Rais Magufuli amesema anafurahi kuona
sasa wakimbizi wa Burundi waliokuwa wamepata hifadhi Tanzania wameanza
kurudi nchi kwao.
Rais
Magufuli pia amefanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa
Tanzania, Benjamin William Mkapa ambaye ni mratibu wa mazungumzo ya
amani ya mgogoro wa Burundi aliyealikwa kuhudhuria mkutano wa 19 wa
wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hapa Kampala.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment