Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Tuesday, 30 January 2018

REA III YAZINDULIWA KIBONDO, KAKONKO

 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Nne kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Br. Gen. Mstaafu Emanuel Maganga (wa Tano kushoto), Mbunge wa Muhangwe ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye (wa pili kushoto), Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (wa Kwanza kushoto) wakifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu katika wilaya za Kibondo na Kakonko.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati), Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Br. Gen. Mstaafu Emanuel Maganga (wa Tano kulia), Mbunge wa Muhangwe ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye (wa Tano kushoto), Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (wa Tatu kushoto) Wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa Usambazaji mradi wa umeme vijijini Awamu ya Tatu katika wilaya za Kakonko na Kibondo mkoani Kigoma.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa Tatu kulia), akimkabidhi kifaa cha UMETA mmoja wa wananchi katika kijiji cha Mabamba wilayani Kibondo. Kifaa hicho kitamwezesha kuwasha umeme ndani ya nyumba bila kufunga nyaya za umeme. Wa Pili kulia ni Mbunge wa Muhangwe ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi (wa pili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Dkt Gidion Kaunda (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Mhandisi Bengiel Msofe (wa kwanza kushoto), wakisaini vitabu vya wageni katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kibondo mara walipofika wilayani humo kwa ajili ya uzinduzi wa mradi wa usambazaji umeme vijijini uliofanyika wilayani Kibondo mkoani Kigoma.
Baadhi ya wananchi katika kijiji cha Mabamba wilayani Kibondo wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ( hayupo pichani) wakati alipofika kijijini hapo kuzindua mradi wa usambazaji umeme vijijini awamu ya Tatu.
**************
Na Teresia Mhagama, Kigoma
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amezindua mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu katika wilaya za Kakonko na Kibondo mkoani Kigoma ambapo vijiji 69 vya wilaya hizo vitaunganishiwa umeme.

Uzinduzi huo umefanyika katika kijiji cha Mabamba wilayani Kibondo na kuhudhuriwa na Mkuu wa mkoa wa Kigoma, watendaji wa Wilaya , Halmashauri, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mbunge wa Muhambwe, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mbunge wa Buyungu na wananchi.

Akizindua Mradi huo, Dkt. Kalemani alisema kuwa katika wilaya ya Kibondo vijiji 40 vitasambaziwa umeme na katika wilaya ya Kakonko jumla ya vijiji 29 vitapata umeme na kueleza kuwa vijiji vitakavyosalia vitasambaziwa umeme kuanzia mwezi Julai, 2019.

Aliongeza kuwa, Mkandarasi atakayesambaza umeme katika wilaya hizo ni kampuni ya Urban & Rural Engineering ambapo jumla ya shilingi bilioni 25 zitatumika katika kazi hiyo.

Dkt. Kalemani alitumia fursa hiyo kuwaagiza watendaji katika Halmashauri nchini kutenga fedha kwa ajili ya kufunga miundombinu ya umeme katika Taasisi za Umma na sehemu zinazotoa huduma za kijamii kama Shule, Vituo vya Afya, Visima vya Maji, sehemu za Ibada na masoko ili mkandarasi atapofika katika eneo husika aweze kuweka umeme.

Aidha, alitoa maagizo kwa wakandarasi wa umeme vijijini kukamilisha kazi ndani ya wakati, wasiruke vijiji na pia waajiri vijana wa eneo husika wakati wa utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Br. Gen. Mstaafu Emanuel Maganga aliishukuru Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo ambao mwananchi anagharamia shilingi 27,000/= ili kuunganishwa umeme huku gharama nyingine zikibebwa na Serikali.

Aidha, alitoa maagizo kwa watendaji wa Wilaya na Halmashauri za mkoa wa Kigoma kuhakikisha kuwa wanamsimamia Mkandarasi huyo katika hatua zote za utekelezaji wa mradi ili afanye kazi kulingana na mkataba wake.

Mbunge wa Muhambwe ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye pamoja na kupongeza juhudi za Serikali kupeleka Umeme katika Vijiji hivyo, aliisisitiza REA kuhakikisha kuwa vijiji ambavyo bado havijaingizwa katika mpango wa kupelekewa Umeme katika mzunguko wa kwanza, navyo pia visambaziwe nishati hiyo.

Aidha, Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago alizungumzia gharama za kufunga nyaya za umeme ndani ya nyumba ambazo alieleza kuwa ni kubwa, " nakushauri Waziri wa Nishati, uwaelekeze wakandarasi wanaofanya kazi ya kufunga nyaya za umeme waache kuweka gharama za kutisha," alisema.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment