Na Hellen Mlacky
WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeuza meno ya viboko vipande 12,467 vyenye uzito wa tani 3.5 (kilo 3,580.29 ) kwa Sh milioni 30.9 katika mnada wa hadhara uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Aliyeibuka mshindi katika mnada huo ni Lorey Kilasi wa kampuni ya Ontour Tanzania Ltd ambaye alilipa asilimia 25 ya fedha hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kabla ya mnada huo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ulinzi wa Wanyamapori TAWA, Mabula Misungwi alisema mnada huo ulishirikisha kampuni 19 zenye leseni daraja la kwanza.
“Sisi hapa ni kama waangalizi kwa sababu anayefanya kazi hii ya mnada ni Kamati Maalum inayojumuisha watu kutoka Wizara ya Fedha na ndiyo wasimamizi wakuu…Utaratibu ni kwamba meno yanakusanywa na yanaletwa hapa kidogo kidogo na mara ya mwisho uuzaji kama huu ulifanyika 2004” alisema.
Alisema meno hayo siku za nyuma kuna kampuni zilizokuwa zimesajiliwa zinafanya kazi hiyo ya ununuzi ila kwa sasa utaratibu umebadilika badala ya kuziuzia moja kwa moja unafanyika mnada wa hadhara.
“Mnada huu unahusisha wafanyabiashara wa nyara waliopewa leseni ya nyara daraja la kwanza mwaka 2017... meno haya yanatumika kama urembo, wengine wanayasaga kutengeneza sanamu na soko lake kubwa lipo Ulaya” alisema.
Alisema mnunuzi huyo aliyeshinda amelipa asilimia 25 ya malipo hayo papo hapo na asilimia 75 iliyobakia atatakiwa kulipa ndani ya siku 14 zijazo baada ya mnada huo.
Mapema Mwenyekiti wa mnada huo kutoka Wizara ya Fedha, Karerema Kwaleh alitangaza kwamba meno hayo yatauzwa kwa wastani wa uzito wa nusu kilo bila kugawanywa au kuchambuliwa wakati wa mnada na wanunuzi wataruhusiwa kuondoa bidhaa kwenye eneo la mnada baada ya kulipia ada na kodi husika kikamilifu na kupewa hati ya kumiliki nyara hizo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment