Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango ametoa maagizo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza
kuwa utekelezaji wake uanze tarehe 1
Januari, 2018. Maagizo hayo ni kama ifuatavyo:
-
i.
Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi
ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi, bei ya
ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya
kielektroniki.
ii.
Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au
wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake
yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za
usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini
kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, na gharama
za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni
watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili
kwa makampuni.
iii.
Viwango vya kubadilishana fedha
vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na
visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni mabenki na maduka ya fedha za
kigeni tu yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na
ushindani katika soko la fedha za kigeni.
iv.
Mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia
bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.
Aidha Dkt. Mpango
ameviagiza vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote
watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA FEDHA NA
MIPANGO
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment