Naibu Waziri wa Ujenzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Elias John Kwandikwa (kushoto) akifafanua hoja kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni, Dodoma. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Prof. Norman Sigalla King.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Emmanuel Mwakasaka (anayeongea) akichangia hoja kuhusu Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania uliowasilishwa kwenye Kamati hiyo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Ujenzi, Mhe. Elias John Kwandikwa (hayupo pichani) kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Angelina Madete (aliyekaa katikati) akifuatilia majadiliano ya wadau kuhusu Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni Dodoma.
******************
Serikali imeandaa Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa kuwa inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na iweze kujiendesha kibiashara na hatimaye kutoa gawio kwa Serikali.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Ujenzi, Elias John Kwandikwa (Mb) wakati akijibu hoja za Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania ambao umewasilisha mbele ya Kamati hiyo ambapo wajumbe waliupitia Muswada huo, kutoa maoni, ushauri na mapendekezo ya kuuboresha Muswada. Mawasilisho hayo ya Serikali na majadiliano na wajumbe wa Kamati hiyo yamefanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma.
Kwandikwa ameongeza kuwa lengo la Serikali kuandaa Muswada huo, ni kuiwezesha TTCL kujiendesha kibiashara, kutoa gawio kwa Serikali, kuendana na ushindani wa hali ya soko la mawasiliano nchini na kwa maslahi mapana ya taifa kwa kuzingatia kuwa TTCL inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Muswada huu utakapokamilika na kuwa Sheria itaiondoa TTCL kwenye Sheria ya makampuni na kuwa chini ya Sheria ya mashirika ya umma na hivyo kuifanya TTCL kuwa Shirika na sio Kampuni tena.
Katika kikao hicho, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imepokea hoja kutoka kwa Kamati hiyo za kuboreha Muswada huo. Hoja zilizopokelewa ni hoja 26 zenye makosa ya kiuandishi zinazohusu Muswada huo ambapo zitafanyiwa marekebisho na hoja mahususi nne zilizojikita kwenye kifungu cha 7(5) na 7(7) kinachozungumzia wajumbe wa Bodi, kifungu cha 9(1) kinachohusu mamlaka na maelekezo ya Waziri mwenye dhamana kwa Bodi na kifungu cha 15(3)(b)kinachohusu kigezo cha uzoefu wa uongozi wa mtendaji mkuu wa shirika wa angalau miaka 8 ya atakayeteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu ambazo zimetolewa ufafanuzi na Mhe. Kwandikwa kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa.
Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeridhia Muswada huo ikiwa ni pamoja na majibu ya Serikali ya hoja 26 za Kamati zenye makosa ya kiundishi, hoja moja ya kifungu cha 7(5) kati ya hoja nne mahususi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Norman Sigalla King ameieleza Serikali kuwa msimamo wa Kamati yake ni kuitaka Serikali ipunguze muda wa uzoefu wa uongozi wa mtendaji mkuu wa shirika kutoka kigezo cha muda wa angalau miaka minane na kuwa miaka mitatu kama ilivyo kwenye kifungu cha 15(3)(b).
Naye Kwandikwa aliieleza Kamati kuwa Serikali kupitia sheria na kanuni zake za utumishi wa umma na suala zima la uendeshaji wa mashirika ya umma ni vema kigezo cha uzoefu wa mtendaji mkuu wa shirika ukawa angalau miaka 8 kama kifungu cha 15(3)(b) kilivyoainisha ili kumuwezesha kuwa na weledi, ujuzi na uzoefu wa kutosha kuendesha shirika la umma ambalo linamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Katika hatua nyingine Kwandikwa alieleza Kamati kuwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Shirika la Mawasiliano Tanzania ataendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu ya shirika kupitia wajumbe wa bodi ya shirika kwa kutoa maelekezo ya jumla au maalumu kama ilivyoelekezwa kwenye kifungu cha 9(1) cha Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania, “kifungu hiki ni muhimu kwa, Waziri kwa kuwa Serikali ina miliki shirika kwa asilimia 100, linatakiwa lijiendeshe kibiashara na kutoa gawio kwa Serikali”. “Aidha, tumeshuhudia kuwa Serikali ina mashirika 64 ambapo ni mashirika kumi na moja tu yanatoa gawio kwa Serikali. Hivyo, Serikali haiko tayari kuona mashirika yake yanajiendesha kwa hasara”, amesema , Kwandikwa.
Kwandikwa ameongeza kuwa tumeshuhudia katika jitihada mbalimbali za Serikali za kuimarisha TTCL hivi karibuni, Serikali kupitia Msajili wa Hazina imeifutia TTCL deni ililokuwa inaidai la shilingi bilioni 76.6 na kuufanya mkopo huo kuwa mtaji ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ushindani, kuongeza mtaji zaidi wa uendeshaji.
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) iliundwa kwa Sura ya 304 na kusajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni, Sura 212 ambapo Muswada huu utakaporidhiwa na kuidhinishwa TTCL itakuwa Shirika la umma kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment