Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza hii leo wakati wa kuzindua rasmi usambazaji wa vifaa mbalimbali vya maabara za Sayansi katika shule za Sekondari 1,696 nchini na kuagiza TAMISEMI kuhakikisha shule zote nchini zinakamilsha ujenzi wa maabara zake haraka.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikabidhi moja ya vifaa vya kufundishia masomo ya Sayansi kwa mmoja wa walimu waliohudhuria.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katikati akizundua.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pia alipata fursa ya kuangalia maonesho ya kisayansi yaliyoandaliwa na wanafunzi na walimu kutoka shule mbalimbali za Sekondari
****************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi Rais (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene ahakikishe
Halmashauri zote zinakamilisha ujenzi wa maabara za sayansi ili vifaa
vilivyoletwa visikae bohari kwa muda mrefu.
“Vifaa vya maabara
vitatolewa katika shule za Tanzania Bara zilizokamilisha majengo na miundombinu
muhimu ya maabara. Hivyo, ni vizuri sasa Halmashauri zote ambazo shule zake
hazijakamilisha ujenzi wa maabara ziongeze bidii ili ziweze kunufaika na
utaratibu huu. Mheshimiwa Waziri wa Nchi TAMISEMI simamia suala hili,” amesema.
Ametoa agizo hilo leo (Jumanne,
Juni 6, 2017) wakati akizungumza na viongozi, walimu na wanafunzi wa shule za
sekondari wanaosoma masomo ya sayansi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa
usambazji wa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari Tanzania bara
iliyofanyika kwenye viwanja vya Lugalo jeshini, jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu pia alimwagiza
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ahakikishe anawasiliana
na Waziri mwenzake wa Zanzibar ili wabadilishane uzoefu na utaratibu huo uweze
kuzinufaisha pande mbili za Muungano.
“Tunapoimarisha
elimu nchini ni vizuri jitihada hizi zikahusisha pande zote mbili za Muungano.
Hivyo, wekeni utaratibu wa kubadilishana uzoefu na wenzetu wa Zanzibar, ili
jitihada hizi zinufaishe pande zote mbili za Muungano,” amesema.
Akizindua
mpango huo, Waziri Mkuu amesema usambazaji wa vifaa hivyo
ni kwa ajili ya shule 1,696 za sekondari nchini ambazo zilikamilisha ujenzi
kabla ya tarehe 30 Desemba mwaka jana.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu
kuhutubia hadhira hiyo, Prof. Ndalichako alisema ununuzi wa vifaa hivyo
umegharimu sh. bilioni 16.9 kutokana na michango ya washirika wa maendeleo kutoka
Benki ya Dunia, Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa (DfID) na Shirika
la Misaada ya Maendeleo la Sweden (CIDA).
Alisema usambazaji wa vifaa
hivyo utafanyika kwenye kanda 11 za kielimu na utahusisha shule za wananchi
1,625 na shule kongwe 71. “Wizara ya Elimu imenunua vifaa hivyo chini ya programu
ya Lipa Kulingana na Matokeo. Vifaa hivi, vinakidhi ufundishaji kwa vitendo kwa
asilimia 100 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita,” alisema.
Naye Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi alisema Jeshi la Wananchi wa
Tanzania litahakikisha linavisambaza vifaa hivyo katika kanda zote 11
zilizoteuliwa.
Akifafanua kuhusu maghala
ya jeshi kutumika kutunzia vifaa hivyo na kemikali, Dk. Mwinyi alisema Serikali
imepata unafuu mkubwa kwa kutumia maghala hayo na hivyo kuokoa fedha ambazo
zingetumika kulipia sehemu nyingine.
Naye Mshauri wa Elimu
kutoka DfID, Bi. Tanya Zebroff akitoa salamu kwa niaba ya washirika wa
maendeleo alisema wamefurahi kupata fursa ya kuisaidia Seriakli ya Tanzania na
watoto wa Kitanzania katika suala la elimu.
Tulipata fursa ya
kutembelea mabanda na kuangalia vifaa vya maabara vilivyooneshwa, pia tumezungumza
na wale watoto. Tumeona hamasa waliyonayo watoto wale ambao ni wanasayansi wa
siku zijazo, tumefarijika sana,” alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment