Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Tuesday 6 June 2017

MFUMO MPYA WA UHASIBU NA UTOAJI TAARIFA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Katibu Tawala mkoa wa Dodoma, Rehema Dendegu akifungua mafunzo ya siku mbili  ya mfumo mpya wa Uhasibu na Utoaji Taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma  ‘Facility Financial Accounting  and Reporting System – FFARS katika ukumbi wa LAPF Conference Centre Dodoma.



Nyaborogo Patrick Marwa, Mhasibu wa Afya Halmashauri ya Wilaya  ya Chamwino akichangia wakati wa mafunzo ya mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma ‘Facility Financial Accounting  and Reporting System – FFARS.




Mkuu wa kitengo cha Mifumo ya Fedha wa Mradi wa PS3, Dkt. Gemini Mtei,  akielezea lengo la mafunzo  ya mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma ‘Facility Financial Accounting  and Reporting System – FFARS.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma ‘Facility Financial Accounting and Reporting System – FFARS wakifanya mafunzo kwa vitendo baada ya maelekezo kutoka kwa wakufunzi. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.


Mwezeshaji wa mafunzo ya mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma ‘Facility Financial Accounting and Reporting System – FFARS, Abdul Kitula, Mshauri wa Udhibiti wa Fedha za Umma wa mradi wa PS3 akifundisha washiriki namna ya kutumia mfumo huo
                                                                            ***************
SERIKALI sasa itaanza kupeleka rasilimali fedha moja kwa moja kwenye vituo vya afya kwa ngazi za halmashauri ikiwa ni moja ya jitihada za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.  Anaandika Mroki Mroki wa Daily News-Habarileo Blog.

Upelekaji wa Rasilimali Fedha moja kwa moja kwa vituo vya kutolea huduma itahakikisha kuwa Fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Mkakati huu mpya wa kuboresha sekta ya afya unatekelezwa kwa njia ya msaada kutoka Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).

Vituo vya kutolea huduma ambavyo vitapokea fedha hizo vinajumuisha Zahanati, Vituo vya Afya, na Hospitali za Wilaya.  Zoezi hili ni sambamba na inavyotekelezwa kwenye sekta ya elimu, Serikali za Vijiji na Ofisi za Kata.

Mfumo huu mpya wa kupatiwa rasilimali fedha utatoa motisha kwa vituo vya kutolea huduma za afya na kuongeza kipaumbele cha utoaji huduma bora kwa wananchi wa Tanzania na kuongeza usawa na uwazi.  

Aidha kupitia mfumo huo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS) unasaidia utekelezaji wa utoaji wa rasilimali fedha moja kwa moja kwa ngazi za vituo vya kutolea huduma kwa kuimarisha uhitaji wa kuwepo kwa usimamizi wa fedha katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma.  

FFARS itawapatia watoa huduma mfumo sanifu uliorahisishwa ambao utawawezesha kutunza taarifa za fedha zinazotolewa na zilizopo katika vituo vyao.  

FFARS itaweza kufuatilia matumizi ya fedha hizo katika kufikia malengo ya utohaji huduma na kuhakikisha yanaendana na sheria za manunuzi na utoaji taarifa.  Taarifa hizi zitasaidia Serikali kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma na kuongeza uwazi, na hivyo watoa huduma wa afya kuwa na wajibu kwa jamii wanayoihudumia.

Sambamba na uzinduzi wa FFARS, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), wameandaa mafunzo ya kina yatakayoanza mwezi huu kwa wakufunzi 490 katika ngazi ya taifa na halmashauri, yatakayofanyika katika mikoa minne nchini.

Mikoa ambayo itahusika katika mpango huu ni  Dodoma, Mbeya, Mtwara, na Shinyanga, ambao utawawezesha watumishi katika vituo vya Afya na Elimu kupata ujuzi wa namna ya kutumia mfumo mpya wa FFARS.  

Wakufunzi wataweza kutoa elimu ya utumiaji wa mfumo huo kwa watumiaji wa mwisho wa mfumo wa FFARS kwa zaidi ya Vituo vya Afya 550, Zahanati 6800, Hospitali za Wilaya 135, na takribani Shule za Msingi na Sekondari 20,000 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, vikiwemo vituo vya kutolea huduma kutoka Mikoa 13 na Halmashauri 93 zinazotekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).

Mafunzo haya yatahakikisha kuwa watoa huduma katika vituo wana ujuzi unaohitajika katika usimamizi wa fedha na kutoa  huduma bora kwa wananchi wote Tanzania na kwa jamii zenye uhitaji.

Mwongozo huu wa FFARS upo katika aina mbili: mfumo wa kielektroniki, na mfumo wa zamani ulioboreshwa wa kujaza katika vitabu kulingana na miundombinu iliyopo katika vituo vya kutolea huduma Tanzania nzima.  

Ufahamu uliopo katika kutumia mfumo wa zamani utasaidia uelewa wa haraka katika kutumia mfumo wa kielektroniki, na baada ya uboreshwaji wa miundombinu tunatarajia vituo vyote vitahamia katika mfumo wa kielekroniki.

Mfumo huu wa FFARS unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI); Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi; na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na USAID. 

Mfumo utatumika katika vituo vyote vya kutolea huduma ya afya na shule, na uhuishaji huu wa mfumo utarahisishia na kuongeza ufanisi katika mifumo ya Serikali ya Tanzania na kuboresha usimamizi na matumizi ya rasilimali za umma.

Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3), ni wa miaka mitano na unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania bara.  PS3 inafanya kazi katika sekta mbalimbali ili kuimarisha mifumo ya mawasiliano, utawala bora, fedha na rasilimali watu, hususani kwa jamii zenye uhitaji.


2 comments:

  1. Mfumo huu ni mzuri sana kwani utarahisha watumishi wanaosimamia raslimamli fedha katika vituo vya kutolea huduma kutoa taarifa kwa wakati na zilizo hahihi.
    ushauri hadi sasa bado watumiaji wa mfumo huu hawajawa na uwezo wa kuutumia kwa usahihi hii ni kutokana na wengi kutopata mafunzo ya kutosha namna ya kuutumia, baada ya mfumo huu kuboreshwa na kuwepo na chngamoto ya bakaa kuhama kutoka kwenye mifuko iliyobajetiwa na mfumo ulikubali na kuruhusu malipo kufanyika hata kama fedha hakuna. kwa sasa mfumo umetengemaa lakini wengi anashindwa kulipa kwa kuonekana hakuna fedha. Hivyo utatuzi umepatikana lakini wengi wanahoitaji mafunzo zaidi.

    ReplyDelete
  2. Nawapongeza wote waliotengeneza Mwongozo wa kufundisha FFARS kwa kutumia video nzuri kwa kweli nimejifunza na imenisaidia sana

    ReplyDelete