Mkutano mkuu wa mwaka wa Shirikisho la wakuu wa Polisi kwa
nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) unatarajia kufanyika Mei 24, 2017 mkoani
Arusha chini ya mwenyekiti wa Shirikisho hilo kipindi hiki ambaye ni Mkuu wa
Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu (pichani).
Mkutano huo utatanguliwa na
mikutano ya kamati tendaji za SARPCCO kabla ya kufunguliwa rasmi Mei 24, 2017 na Waziri wa Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba ambapo mambo mbalimbali
yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa
kufanya Operesheni za pamoja katika kubaini na kukabiliana na makosa mbalimbali yakiwemo dawa za kulevya, wizi wa magari, usafirishaji
haramu wa binadamu na ugaidi.
Vilevile, mkutano huo
utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na Wakuu wa Upelelezi wa SARPCCO
pamoja na kamati tendaji za sheria, Mafunzo na kamati tendaji ya Jinsia na
watoto katika mkutano wao uliofanyika mwezi Machi mjini Bagamoyo.
Aidha suala la michezo baina
ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama nalo linatarajiwa kujadiliwa katika
mkutano huo.
SARPCCO iliundwa mwaka 1995
kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa
Afrika katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu. Shirikisho hilo linaundwa na
Nchi kumi na tano ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Lesoto,
Mauritius, DRC, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland, Madagascar
na Syshelis.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment