Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (kulia) akitoa hotuba ufunguzi wa
kikao kazi cha mwaka kinachowahusisha maafisa wakuu wa jeshi la Polisi na
makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma.
Baadhi
ya maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi wakiimba wimbo wa maadili ya afisa wa
polisi wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa hao na makamanda
wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi
la Polisi.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (kulia) akiongea na Mkuu wa Jeshi la
Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu wakati
wa hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa wakuu wa jeshi la Polisi na
makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma.
Na Frank Geofray-Jeshi
la Polisi.
Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba amewataka maofisa na askari Polisi kote nchini
kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu ili kujenga taswira nzuri kwa wananchi
wanaowahudumia jambo ambalo litaongeza imani na ushirikiano katika kukomesha
vitendo vya uhalifu nchini.
Waziri Nchemba
ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua kikao kazi cha Maofisa wakuu wa Jeshi
la Polisi kutoka makao makuu, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na vikosi kutoka bara
na Zanzibar kinachoendelea mkoani Dodoma.
Alisema Pamoja na Jeshi
hilo kufanya kazi nzuri bado linakabiliwa na changamoto ya baadhi ya askari na
maofisa wasio waadilifu wanaofanya vitendo vya kuwabambikia wananchi kesi na wakati mwingine
kuwabadilishia kesi ili kujenga mazingira ya kupatiwa rushwa jambo ambalo ni
kinyume na maadili ya askari Polisi.
“Fanyeni kazi kwa
weledi hasa kwa kuwasimamia waliopo chini yenu kwa kuwa wapo baadhi yao bado
hawataki kubadilika na katika awamu hii lengo letu ni kutoa haki kwa maskini
hivyo ninyi kama wasimamizi wa sheria mnapaswa kutenda haki mnapofanya kazi
zenu na wale wasiotaka kubadilika hamna budi kuchukua hatua ” Alisema Nchemba.
Aidha alilitaka Jeshi
hilo kuwachukulia hatua bodaboda wanaofanya makosa na wale wasiokuwa na makosa
waachwe waendelee na majukumu yao ya kujipatia kipato na kuachana na dhana ya
kuwa kila bodaboda ni mhalifu.
Kwa upande wake Inspekta
Jenerali wa Polisi, IGP Ernest Mangu alisema kikao hicho kinafanyika kwa siku
tatu kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka uliopita na
kuweka mikakati kwa mwaka huu ili kuendeleza juhudi za kukabiliana na vitendo
vya uhalifu hapa nchini.
Mangu alisema Jeshi
hilo litaendelea na Oparesheni zake za kupambana na uhalifu zikiwemo za dawa za
kulevya, uhalifu wa kutumia silaha na wizi wa mtandao kwa mikakati mipya ambayo
itaibuliwa katika kikao kazi hicho ili kuhakikisha hakuna mhalifu anayetamba
hapa nchini.
Naye Mwenyekiti wa
Kamati ya kudumu ya Bunge mambo ya nje na usalama Balozi Adadi Rajabu alisema
kamati hiyo itaendelea kuishawishi Serikali kuboresha maslahi na vitendea kazi
vya Jeshi la Polisi ili Jeshi hilo liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Ufunguzi wa Kikao kazi hicho
ulihudhriwa pia na Waziri Mkuu mstaafu Samweli Malechela, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Jordan Rugimbana pamoja na baadhi ya wabunge na Kamati ya ulinzi na usalama ya
mkoa wa Dodoma.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment