Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na kutoa maagizo mbalimbali
kuhusu makontena 20 (yanayoonekana nyuma) yenye mchanga wa madiniuliokuwa usafirishwe
kwenda nje ya nchi ambapo ameagiza Kontena hizo zisisafirishwe mahali popote.
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika ziara ya kushtukiza
katika Bandari ya Dar es Salaam kufatilia maagizo yake ya kudhibiti vitendo vya
udanganyifu vinavyofanywa na wafanyabiashara wanaogiza na kusafirisha mizigo
ndani na nje ya nchi.
Makontena 20 yenye mchanga wa
madini yakiwa yamezuiwa kusafirishwa nje ya nchi na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mara alipofanya ziara ya kushtukiza
katika bandari ya Dar es Salaam.
*************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 23 Machi, 2017 amefanya ziara
ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kufuatilia
utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu
wa mizigo inayoingia na kutoka nchini kupitia bandari hiyo ikiwemo usafirishaji
wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi.
Katika ziara hiyo Mhe. Rais
Magufuli ameshuhudia makontena 20 ya mchanga wenye madini kutoka kwenye migodi
iliyopo kanda ya ziwa ambayo yamezuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu
alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi tarehe 02
Machi, 2017.
Pamoja na kushuhudia makontena
hayo, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP - Ernest
Mangu na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga wa madini unashikiliwa
popote ulipo, mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli.
“Nataka niwaambie nchi yetu
inachezewa mno, nimekuja kuyaona haya makontena kama yapo, na kweli nimeyaona,
sasa utaratibu utakapokamilika nataka Watanzania na dunia nzima ione kilichomo
humu ndani kama ni mchanga kweli ama dhahabu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa bandarini hapo Mhe. Dkt.
Magufuli pia ameshuhudia udanganyifu mwingine unaofanywa na wafanyabiashara
wanaoagiza mizigo kutoka nje ya nchi baada ya kuoneshwa makontena ambayo
nyaraka zinaonesha yamebeba mitumba ya nguo na viatu wakati ndani yake kila
kontena moja limebeba magari matatu ya kifahari.
Maafisa wa bandari ya Dar es
Salaam na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa
kufuatia maelekezo aliyoyatoa ya kuhakikisha mizigo yote inakaguliwa kwa
mitambo ya mionzi (Scanning Machines) wamefanikiwa kubaini udanganyifu mwingi
unaofanywa na wafanyabiashara wanaoingiza nchini na kusafirisha nje ya nchi
mizigo mbalimbali yakiwemo makontena 10 ambayo yamepatikana yakiwa na magari ya
kifahari ilihali nyaraka zake zikionesha yana mitumba ya nguo na viatu.
Mhe. Rais Magufuli
amewapongeza maafisa na wafanyakazi wa bandari ya Dar es Salaam na TRA kwa kazi
nzuri wanayofanya kudhibiti upotevu wa fedha za umma bandarini hapo na
amewataka kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa uzalendo na kujiepusha na rushwa.
“Leo mmenifurahisha sana,
ninawatia moyo endeleeni kuwakamata wote wanaofanya udanganyifu huu na
muwachukulie hatua kali za kisheria, lakini msimuonee mtu na msipokee rushwa,
tunataka watu wajifunze kuwa hapa sio shamba la bibi” amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, ametoa wito kwa vyombo
vyote vinavyoshughulikia udhibiti wa mizigo inayoingia na kutoka kupitia
bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine hapa nchini, kuendelea
kushirikiana ili kukomesha vitendo vyote vya udanganyifu ambavyo vinasababisha
nchi kupoteza mapato mengi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment