Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Thursday 2 March 2017

RAIS DKT MAGUFULI APIGA MARUFUKU KUSAFIRISHA MCHANGA WA MADINI NJE YA NCHI



Rais wa Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing mara baada ya kuweka jiwe la Msingi katika Kiwanda kikubwa cha kutengeneza Vigae(Tiles ) cha Good Will kilichopo katika kijiji cha Mkiwa, Mkuranga mkoani Pwani. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vigae laki nane kwa siku na mwekezaji ametumia zaidi ya Dola mil.50 katika uwekezaji huo.



Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing   akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kiwanda hicho cha vigae kilichopo Mkiwa Mkuranga mkoani Pwani.



 Rais Dkt. John Pombe Magufuli akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwakilishi wa Kiwanda hicho cha y Vigae cha Good Will, Huang Heng Chao  kutoka kwa Kiwandani hapo.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited kilichopo katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.

Kiwanda hicho kikubwa Afrika Mashariki na Kati ambacho ujenzi wake umegharimu Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku, kitazalisha ajira za moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 2,000.

Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema pamoja na kiwanda hicho, tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani jumla ya viwanda 2,169 vinavyojumuisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na vipo katika hatua mbalimbali za kukamilika.

Nae Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo juhudi za kukuza uchumi zilizowezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi kubwa Barani Afrika na amebainisha kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza uwekezaji nchini Tanzania ikiwemo kujenga viwanda.

"Mhe. Rais kwa mujibu wa takwimu za TIC mpaka mwisho wa Juni 2016 uwekezaji wa moja kwa moja kutoka China umefikia Dola za Marekani Bilioni 6.6 na umezalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 150,000 na zisizo za moja kwa moja 450,000 na kiwanda hiki cha Goodwill Tanzania Ceramic Limited kimejengwa na wawekezaji kutoka China, vipo viwanda vingine vingi vinajengwa, Mbunge wa Mkuranga ameniambia kuwa kuna viwanda zaidi ya 50 vya Wachina vinavyojengwa hapa Mkuranga, nimefurahi sana kuona karibu kila sekta Watanzania wanafurahia ushirikiano wa Tanzania na China" Amesema Balozi Dkt. Lu Youqing.

Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Menejimenti ya kiwanda hicho kwa uwekezaji huo na ameelezea kufurahishwa kwake na kutumika kwa teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae.

Kufuatia kujionea mwenyewe teknolojia hiyo, Dkt. Magufuli amepiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi na ametaka mchanga wote ufanyiwe uyeyushaji hapa hapa nchini.

"Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Baada ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited Mhe. Rais Magufuli ameendelea na ziara yake kwa kuzungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi huu na pia amepiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.

Mhe. Rais Magufuli pia amepokea kero za wananchi wa Somanga, Nangurukuru na Mchinga Moja na huko kote amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha huku akiweka bayana kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.

"Najua mmezoea kusikia maneno mazuri mazuri kuwa hakuna atakayekufa kwa njaa, sasa mimi nasema usipofanya kazi, usipolima mazao na kupata chakula wakati mvua inanyesha Serikali haitatoa chakula cha bure kwa wenye njaa, ni lazima tufanye kazi, sasa hivi mvua zinanyesha limeni mazao ya chakula" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji iliyoanza kuibuka mkoani humo, ameahidi kutoa Shilingi Milioni 20 kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Somanga, amewaagiza Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kujenga kituo cha mabasi cha Nangurukuru na pia amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mhe. Hamidu Bobali kuhakikisha anapeleka Daktari katika kijiji cha Mchinga Moja ili kutatua kero ya wananchi kukosa huduma ya matibabu.

Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake kesho Machi 03, 2017  Mkoani Lindi.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment