Na Lilian Lundo – MAELEZO Dodoma
Waziri
wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye (pichani) amesema kuwa wasanii na watu
wenye majina makubwa ndio wanaoonekana zaidi katika athari za madawa ya kulevya
ingawa wapo wengi katika jamii wanayotumia dawa hizo.
Nape
ameyasema hayo Mjini Dodoma alipokuwa akitoa
majibu kwa waandishi wa habari waliotaka kujua namna ambavyo wizara yake
imelipokea sakata la kukamatwa kwa wasanii ambao wanatuhumiwa kutumia madawa ya
kulevya.
“Kama
wizara inayosughulikia suala la wasanii tunaunga mkono juhudi zozote za
kupambana na jambo hili kwa sababu mwisho wa siku sehemu ya wadau wetu
wanaathirika, hivyo basi juhudi za kupambana nalo zinaokoa wadau wetu,”
alifafanua Nape Nnauye.
Aliendelea
kwa kusema kuwa kama wizara inayosimamia wasanii wamekuwa wakijadili na kuzungumza
juu ya athari hizo za madawa ya kulevya kwa wasanii, aidha wapo wasanii ambao
Serikali imewasaidiwa kupata matibabu kutokana na athari za madawa hayo,
akiwemo mwanamuziki Rehema Chalamila anayefahamika kama Ray C.
Aidha
amesema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa huo hivyo hawajibiki kuuliza Wizara hiyo anapotaka
kuchukua hatua zozote kwa wasanii waliopo ndani ya mkoa anaosimamia, lakini
anapohitaji anaweza kuiuliza wizara hiyo.
Nape
amesema kuwa ni kazi kubwa sana kwa mtu kutengeneza jina (brand) lakini ni rahisi sana kubomoa, hivyo basi ni
vyema busara ikatumika katika kuwashughulikia waathirika, vile vile watu
wasihukumiwe kwa tuhuma.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitangaza majina ya watu wanaotuhumiwa kuuza ama kutumia madawa ya kulevya wakiwemo wasanii, maaskari na wafanyabiashara na kuwataka kuripoti Polisi kwa ajili ya mahojiano.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment