Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah
Kairuki, akizungumza Bungeni Mjini Dodoma.
Na Lilian Lundo – MAELEZO - DOdoma
Serikali
imesema kwamba itafanya uchunguzi juu ya changamoto na matatizo ambayo
yamejitokeza katika mradi wa TASAF ili kuja na mfumo mwingine bora zaidi kwa
ajili ya wanufaika wa mradi huo.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah
Kairuki ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa
taarifa ya Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2016/2017 ambapo wabunge
waliulalamikia mradi huo kuwa na matatizo katika maeneo ambayo wanayasimamia.
Angellah
Kairuki alisema kuwa wizara yake itafuatilia changamato zote ambazo wabunge
wamezianisha ikiwemo utoaji wa fedha kwa kaya ambazo hazina sifa, matumizi
mabaya ya fedha za mradi kwa baadhi ya wanufaika pamoja na usimamizi mbovu wa
fedha za mradi kwa watendaji wa Halmashauri.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Jimbo la Nzega Hussein Bashe ameishauri Serikali kutafuta
mfumo mzuri wa kuzitoa fedha hizo ili wanufaika waweze kuzitumia kwa kuanzisha
biashara ndogondoga ambazo zitawasaidia kujikimu na kuziendeleza familia zao
kiuchumi.
Aliendelea
kwa kusema kuwa, kuwe na utaratibu wa wanufaika kutoa mchanganuo wa namna
walivyozitumia fedha hizo ili kuleta nidhamu kwa wanufaika wanaotumia fedha
hizo kinyume na malengo yaliyowekwa.
Aidha,
Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdallah Chikota amesema kuwa katika jimbo lake
kuna kaya ambazo zimetolewa katika mradi huo kwa kukosa sifa. Kaya hizo
zimeagizwa kurejesha fedha zote ambazo walipatiwa kupitia mradhi huo, na wengi
wao hawana uwezo wa kurejesha fedha hizo.
Hivyo
basi, ameiomba Serikali kuwachukulia hatua Waratibu wa Mradi huo kwani ndio
waliotoa fedha kwa watu wasio na sifa, badala ya kuwaambia wananchi kurejesha fedha
walizopewa kwani wengi wao hawana huwezo
wa kuzirejesha kutokana na vipato vyao kwa vya chini.
Akiwasilisha
taarifa ya Kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Pudenciana
Kikwembe amesema kuwa, mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini nchini
umeonyesha mafanikio makubwa, licha ya kasoro kadhaa zinazotokana na baadhi ya
Watendaji wa Halmashauri wanaohusika kukosa uwazi na uadilifu katika
uwajibikaji wao.
Hivyo
basi, hali hiyo imesababisha kubainika kwa Kaya 55, 692 zisizo na sifa stahiki lakini zilikuwa zikinufaika na mpango hu o wa
kunusuru Kaya Masikini.
Aidha
Kamati imeishauri serikali kuimarisha uwezo wa Halmashauri katika kusimamia
miradi ya TASAF ili itekelezwe kikamilifu na kwa ufanisi pamoja na kuimarisha
mifumo ya kuwatambua walengwa wa Mpango huo na kuzuia kaya zisizo na sifa
kunufaika.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment