Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. George
Boniphace Simbachawene akizungumza na baadhi ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa
na Vijiji leo jijini Dar es Salaam kuhusu uamuzi wa Serikali wa kusitisha kwa
muda katazo la Wenyeviti hao kutumia Mihuri ya Ofisi na badala yake utaratibu
wa awali uendelee hadi hapo hatua nyingine zitakapochukuliwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. George
Boniphace Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kusitishwa kwa
muda kwa waraka uliotoa muungozo wa matumizi ya Mihuri kwa Wenyeviti wa
Serikali za Mitaa na Vijiji leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. George
Boniphace Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wenyeviti wa
Serikali za Mitaa wa Mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kumaliza mkutano wake
na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Serikali wa kusitisha kwa muda katazo
la Wenyeviti hao kutumia Mihuri ya Ofisi na badala yake utaratibu wa awali
uendelee kutumika hadi hapo hatua nyingine zitakapochukuliwa.
***************
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Serikali imesitisha waraka
wa muongozo uliotolewa kuhusu matumizi ya mihuri kwa wenyeviti wa Mitaa na
vijiji mpaka pale itakaposhirikiana na kukubaliana namna bora ya kuendesha
masuala ya kuhudumia wananchi.
Akizungumza na baadhi
ya wenyeviti wa mtaa, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene amewataka wenyeviti wa mitaa nchini
kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo.
Mhe.Simbachawene
alisema kuwa nia ya kusitisha waraka huo ni kuweka utendaji mzuri baina ya
Serikali na watendaji wake wa chini.
“Utaratibu uliopo uendelee
mpaka pale Serikali itakapotoa utaratibu mwingine wa matumizi mbalimbali ya
mihuri hiyo baada ya kujadiliwa na kushirikiana vya kutosha” alifafanua Waziri
Simbachawene.
Mhe.Simbachawene
alisema kuwa kuna baadhi ya wenyeviti wa mitaa wamekuwa wakitumia vibaya mihuri
hiyo na kupelekea migongano na migogoro ya ardhi katika vijiji na mitaa ikiwemo
maeneo ya Ununio, Temeke.
Mbali na hayo alisema
kuwa katika Tangazo la Serikali namba 3 lililotolewa 5 Septemba, 1994 limeeleza
baadhi ya vitendea kazi vya mwenyekiti wa mtaa ni bendera yenye nembo ya
Halmashauri, daftari ya kutunza kumbukumbu na rejista ya makazi.
Alisema kuwa mamlaka ya
mwenyekiti haitokani na mihuri, bali utendaji uliopo ndani ya mtaa au kijiji
husika, hivyo mamlaka ya mwenyekiti ipo pale pale na haibemwi na muhuri bali
muhuri huonesha nguvu ya ofisi baada ya kuwashirikisha watendaji tofauti ndani
ya kijiji katika kutoa maamuzi.
“Mhuri si mali ya mwenyekiti binafsi, hivyo
kwa yeyote atakayekiuka matumizi ya mihuri hiyo Sheria itachukua mkondo wake”
alisisitiza Mhe. Simbachawene.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Temeke Bakiri Makele,
ameahidi kushirikiana na Serikali kwa kutumia mihuri hiyo kwa kufuata Sheria na
taraibu zilizopo.
Naye Katibu wa Wenyeviti
hao, Marium Machicha alimshukuru Waziri mwenye dhamana kwa kauli aliyoitoa baada
ya kuliona tatizo hilo na kuahidi kulifanyia kazi.
Serikali ilitoa Muongozo
huo wa namna wa matumizi ya mihuri kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji kwa sababu
ya matumizi mabaya ya mihuri kwa baadhi ya wenyeviti wa mtaa na vijiji nchini.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment