Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na
Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Bw. Erik Solheim ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku 2.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na
Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Bw. Erik Solheim ambaye ameongozana na ujumbe wake kwa ziara ya siku 2 wengine waliohudhuria ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba (kulia) na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Faustine Kamuzora.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba akifafanua jambo wakati wa mkutano wa Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na
Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Bw. Erik Solheim na ujumbe wake .
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameliomba Shirika
la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kuisaidia Tanzania kukabiliana na tatizo kubwa
la uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini ambao umepelekea
mamia ya ekari za misitu kutoweka kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza
mkaa.
Makamu wa Rais
Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Makamu wa
Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema pamoja na Serikali kufanya jitihada kubwa
za kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira ikiwemo mpango wa upandaji
wa miti kote nchini lakini bado msaada na nguvu zaidi inahitajika kutoka
shirika la Mazingira la UNEP ili kuongeza kasi ya kukabiliana na tatizo hilo
nchini.
Amesema
Tanzania ina mahusiano mazuri na ya muda mrefu na Shirika la UNEP ambapo
shirika hilo limeweza kuisaidia nchi katika miradi mbalimbali ya kuhifadhi
mazingira hivyo mahusiano hayo mazuri ni muhimu yakaja na mbinu bora na nzuri
za kuhifadhi mazingira ili kuokoa Taifa lisigeuke jangwa kutokana na uharibifu mkubwa
wa mazingira unaoendelea nchini.
Makamu wa
Rais pia amehimiza wataalamu wa mazingira wajikite zaidi katika kutoa elimu kwa
wananchi watumie nishati mbadala kama gesi na makaa ya mawe ili kudhibiti
tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza
mkaa.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ERIC SOLHEIM amepongeza
jitihada zinazofanywa na Serikali ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira na
kusisitiza kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali Tanzania
katika Uhifadhi wa mazingira nchini.
Mkurugenzi
huyo amesema suala la kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira sio la Serikali
pekee hivyo ni muhimu kwa Serikali kushirikiana ipasavyo na mashirika yasiyo ya
kiserikali katika kupambana na tatizo ili kupata suluhu ya kudumu.
Naye, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira January Makamba amesema
ujio wa Mkurugenzi Mkuu wa UNEP hapa nchini ni fursa ya kipekee ya kufungua na
kuimarisha ukurasa mpya wa mahusiano kati ya Tanzania na UNEP.
Makamba amesema
kuwa Serikali imetengeneza programu mpya Tano za mazingira ikiwemo kupunguza
matumizi ya mkaa ili kuhifadhi misitu,vyanzo vya maji,kushughulikia taka na
kujenga uwezo kama hatua mpya kabisa ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira
nchini.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment