Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga joelson kulia akiwa na Mkuu
wa Wilaya ya Longido Daniel Chongolo wakiwa kwenye bango la uzinduzi wa Operesheni Zagamba 2018.
Operesheni hiyo ni maalum kwa ajili ya
kudhibiti utoroshaji wa mifugo na mazao yake nchini, ambapo kitaifa
ilizinduliwa Namanga kwenye Wilaya ya Longido. Picha na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga joelson kulia akitoa
maelezo ya maana ya Operesheni Nzagamba2018 kwenye bango la uzinduzi wa Operesheni Zagamba 2018.
Operesheni hiyo ni maalum kwa ajili ya
kudhibiti utoroshaji wa mifugo na mazao yake nchini, ambapo kitaifa
ilizinduliwa Namanga kwenye Wilaya ya Longido. Picha na John Mapepele
Na John Mapepele, Arusha
WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema Serikali kila mwaka inapoteza
jumla ya sh bilioni 263 kila mwaka kufuatia kushamiri kwa utoroshaji wa
mifugo nje ya nchi na uingizaji wa mazao ya mifugo usiozingatia sheria
na taratibu za nchi hali inayochangia ushindani usio wa haki kwa
wazalishaji wa ndani ya nchi.
Akizungumza jana kwenye mnada wa
mifugo wa Namanga wilayani Longido mkoani Arusha wakati wa uzinduzi wa
operesheni maalum ya kitaifa ya kudhibiti upotevu wa mapato na usimamizi
wa biashara ya mifugo na mazao yake iliyopewa jina la ‘Operesheni
Nzagamba 2018’ Waziri Mpina alisema operesheni hiyo itamfikia kila mtu
anayejishughulisha na tasnia nzima ya mifugo.
Alisema
operesheni hiyo itafika kwenye minada ya mifugo, bandarini, viwanja vya
ndege, mipakani, kwenye masoko na maduka,supermarket, na machinjioni ili
kujiridhisha na uhalali wa biashara hiyo.
Pia Waziri Mpina
alisema operesheni hiyo imefanikiwa kubaini kuwepo kwa ubabaishaji
mkubwa unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kufanya udanganyifu
katika biashara ya dawa za mifugo,upotevu mkubwa wa mapato na uingizaji
holela wa mazao ya mifugo kutoka nje ya nchi ikiwemo nyama na maziwa
kupitia njia za panya.
Akitolea mfano eneo la Namanga zaidi ya
mbuzi 22,000 zilikamatwa zikitoroshwa kwenda nchini Kenya huku makusanyo
yakiongezeka na kufikia sh milioni 200 kwa muda wa mwezi mmoja tangu
kuanza operesheni hiyo ambapo kwa upande wa Mwanza makusanyo
yameongezeka kutoka sh milioni 17 kwa mwezi na kufikia Sh. Milioni 532.
Waziri
Mpina alisema tathimini ya awali iliyofanywa na wizara yake imebaini
kuwa wastani wa ng’ombe milioni 1.6 hutoroshwa kila mwaka kwenda kuuzwa
nchi za jirani ambapo Serikali hupoteza sh bilioni 56.4 kwa mwaka huku
upande wa ngozi Serikali ikipoteza sh. Bilioni 87.6 kwa mwaka ambapo
kwa upande wa nyama na maziwa Serikali hupoteza zaidi ya sh bilioni 120
kila mwaka
Aidha alionya kuwa mifugo itakayokamatwa ikitoroshwa
kwenda nchi jirani kinyume cha sheria Serikali itafanya maamuzi magumu
ya kutoza faini kubwa ili kuhakikisha watu wote wanafuata sheria ili
mifugo hiyo iweze kunufaisha watanzania wote kupitia mfumo wa ushuru na
kodi.
Kuhusu tozo ya mifugo inayokwenda nchi za nje, Waziri
Mpina alisema msimamo wa Serikali unabaki pale pale ambapo kila ng’ombe
atatakiwa kulipiwa sh 20,000 na Mbuzi sh. 5,000 huku akiruhusu vibali
vya biashara za mifugo vinavyotolewa na halmashauri viendelee kutumika
hadi pale Wizara ya Mifugo na Uvuvi itakapoamua vinginevyo.
Pia
Waziri Mpina alipongeza uamuzi wa kujengwa kwa mnada wa kisasa wa mifugo
katika eneo hilo la uliofadhiliwa na Mradi wa MIVARF na kugharimu sh.
Milioni 782 na kusisitiza kuwa mnada huo utakuwa mkombozi mkubwa kwa
wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo yao.
Kaimu Katibu Mkuu
Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Lovince Assimwe alisema
operesheni hiyo imewezesha kubaini mianya ya upotevu ya mapato
yatokanayo na sekta ya mifugo na kusisitiza kuwa itakuwa endelevu hadi
pale wadau wa sekta hiyo watakapofuata sheria za nchi.
Dk
Assimwe Serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. John Pombe Magufuli
imedhamiria kwa dhati kusimamia sekta ya mifugo ili iweze kutoa mchango
unaostahili kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alimshukuru Waziri Mpina kwa juhudi
kubwa anazofanya za kudhibiti utoroshaji wa mifugo na kumhakikishia
kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo itaendelea kushirikiana
na wizara kuhakikisha mifugo haiendi nje ya nchi kwa njia za panya.
Alisema
maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Mpina atatumia uwezo wake wote
kuhakikisha yanasimamiwa kikamilifu ili kuweza kupata matokeo mazuri
yanatoyarajiwa.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment