Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban(kushoto) akizungumza kwenye mkutano wa Magavana kutoka nchi za Afrika kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini wakati wa Mkutano wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mjini Busan- Korea Kusini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban (katikati) akiwa na baadhi ya Magavana wa nchi za Afrika, kushoto kwake ni Gavana wa Kenya Mhe. Henry Kiplagat Rotich na kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB, Dkt. Nyamajeje Weggoro baada ya kumaliza majadiliano yanayaozihusu nchi wanazoziwakilisha, Mjini Busan- Korea Kusini. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango-Korea)
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeitaja Tanzania kuwa moja ya nchi za Afrika zenye matumizi bora ya fedha zinazofadhiliwa na Benki hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya miundombinu ya barabara na nishati.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayesimamia nchi 7 za Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro wakati wa kikao cha Magavana wa nchi za Afrika kwenye Mkutano wa mwaka wa Benki ya AfDB unaoendelea Mjini Busan, Jamhuri ya Korea ya Kusini.
Dkt. Nyamajeje alisema kuwa changamoto nyingi zinazotokea katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa nchi za Afrika zinatokana na ukosefu wa wataalamu wa fani mbalimbali, jambo linalosababisha miradi mingi kutomalizika kwa wakati hata hivyo Benki ya AfDB inaendelea kuangalia ni jinsi gani inaweza kusaidia kutatua matatizo hayo na kuleta maendeleo chanya kwa nchi za Afrika.
Akizungumza katika Mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Amina Khamis Shaaban, alisema kuwa Serikali ya Tanzania imesawasilisha barua kwa uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, ili iweze kusaidia katika ujenzi wa Uwanja wa ndege ya Msalato Jijini Dodoma na Uwanja wa ndege wa Zanzibar, aidha miradi hiyo ikiridhiwa na kutekelezwa itakua kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi wa Viwanda nchini Tanzania.
Tanzania ni wadau wakubwa katika Benki ya AfDB hivyo inanufaika na mikopo nafuu inayotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile ujenzi wa Barabara za kiwango cha Lami hususani mkoa wa Tabora na pia miradi ya Nishati ya umeme na maji maeneo mbalimbali nchini.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment