Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisikiliza ripoti ya
Mkemia Mkuu wa Serikali , Samwel Manyele
(kulia) ya chunguzi wa Salfa kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay
jijini Dar es salaam Juni 10, 2017. Wapili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Dkt, Mathew Mtigumwe.
Mkemia Mkuu wa
Serikali, Profesa Samwel Manyele akiwasilisha ripoti ya
uchunguzi wa salfa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye Makazi ya
Waziri
Mkuu, Oysterbay jijini Dar es salaam Juni 10, 2017. Kushoto ni Katibu
Mkuu wa
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt Mathew Mtigumwe. Kulia ni
Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti wa Ubora wa Bidhaa, Ofisi ya Mkemia
Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo.
******************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema salfa iliyoingizwa nchini kwenye makontena 211 haina kasoro na inafaa kwa matumizi ya kupulizia kwenye mikorosho.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumamosi, Juni 10, 2017) wakati akizungumza na wajumbe
wa kamati maalum, waagizaji wa salfa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya
Korosho nchini (CBT) kwenye kikao alichokiitisha kwenye makazi yake,
Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
“Bodi
kaandaeni taratibu za kawaida kusambaza salfa kwa wakulima ili waanze
kupuliza dawa hiyo. Wasichelewe kupuliza kwa sababu msimu umeshaanza,”
amesema.
Juni
4, mwaka huu Waziri Mkuu alimuagiza Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof.
Samuel Manyele aende kuchunguza mzigo wa salfa ulioko bandari ya Dar es
Salaam baada ya kutokea mkanganyiko uliosababishwa na ripoti ya TPRI
kuwa ya salfa iliyoingizwa nchini na kampuni ya ETG Inputs Ltd kwa niaba
ya Bodi ya Korosho haijakidhi viwango.
Waziri
Mkuu alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa kuna mkanganyiko
miongoni mwa wakulima juu ya matumizi ya kiuatilifu hicho licha ya kuwa
Serikali ilikwishapokea taarifa ya bodi, na taarifa ya kampuni
iliyotengeneza salfa hiyo na taarifa iliyoletwa na mwagizaji ambayo
imethibitishwa na makampuni matatu ya kimataifa. Aliyataja makampuni
hayo matatu kuwa ni InterTech, Bureau Veritas na SGS.
Akitoa
taarifa ya uchunguzi wao mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele alisema
walifanya uchunguzi kwenye makontena 21 ambayo ni sawa na asilimia 10 ya
makontena yote 211 ili kubaini ubora wake.
“Uchunguzi ulifanyika kwenye maeneo ya purity, acidity na moisture contentskama
ulivyokuwa umeelekeza. Sampuli zilichukuliwa kutoka GALCO Inland
Container Depot iliyoko Chang’ombe ambako ndiko mzigo wa salfa ulioletwa
na kampuni ya ya ETG Inputs Ltd unahifadhiwa,” alisema.
“Kwa
kuzingatia matokeo ya kiuchunguzi wa kimaabara uliofanyika, viwango
(specifications) vilivyowekwa ndani ya mkataba na viwango vya Shirika la
Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kuhusiana na kiuatilifu cha salfa ni
maoni yetu kuwa mzigo wa salfa ulioko ndani ya makasha (containers) 211
unakidhi viwango,” alisema kwenye taarifa yake.
Kwa upande wake, Makamu
Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho nchini, Bw. Maokola Majogo alisema yeye
pamoja na Bodi yake watatekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu na akawataka
wakulima wasisite kutumia salfa hiyo kwani imekwishathibitishwa na
Mkemia Mkuu kwamba haina matatizo.
Naye, Kaimu
Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho nchini, Bw. Hassan Jarufu alisema Bodi
iliagiza salfa kwa kiwango kile kile cha mwaka jana kilichotumiwa na
wakulima na kuleta matokeo mazuri.
“TPRI
walichukua sampuli na kuleta majibu kuwa ina mapungufu, kwa hiyo
tukashindwa kuisambaza. Mheshimiwa Waziri Mkuu alimuagiza Mkemia Mkuu
afanye uchunguzi wake, na sisi tumefurahia matokeo na tunaenda
kutekeleza maelekezo yake ya kututaka tusambaze salfa kwa wakulima,”
alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment