RAIS John Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa
kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa viwanda katika maeneo
yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza thamani ya mazao yao na kuzalisha ajira.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Ikulu
Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waakuu wa Mikoa ya
Tanzania Bara, kikao ambacho kimehudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Mcheche Masaju, Katibu Mkuu Kiongozi , Balozi John Kijazi na baadhi ya
Mawaziri.
Rais Magufuli amesema kila Mkuu wa Mkoa
anapaswa kufanyia kazi fursa za uanzishaji wa viwanda katika eneo lake na
kuhakikisha anashawishi wawekezaji kuzitumia fursa hizo kama inavyofanyika
katika Mkoa wa Pwani ambako tangu Awamu ya Tano iingie madarakani viwanda
vikubwa 83 vimejengwa na vingine kukamilika huku viwanda vidogo zaidi ya 120
pia vikiwa vimejengwa.
Pamoja na hilo Rais Magufuli amewaagiza Wakuu
wa Mikoa kuongeza juhudi za utatuzi wa migogoro ya ardhi ikiwa ni pamoja na
kuharakisha mchakato wa kuwanyang’anya hati za umiliki wa mashamba makubwa
ambayo yanashikiliwa na watu pasipo kuyaendeleza.
“Mashamba yote yaliyotelekezwa, fuateni
taratibu za sheria, yanyang’anyeni wapewe Watanzania ambao wapo tayari
kuyaendeleza, lakini fanyeni jambo hili kwa kufuata utaratibu” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewatahadharisha Wakuu
wa Mikoa hao dhidi ya watu wanaofanya njama za kujimilikisha maeneo makubwa ya
ardhi na kusababisha wakulima na wafugaji kukosa maeneo ya kilimo na malisho na
ametaka wote watakaobainika kufanya njama hizo wafichuliwe na kunyang’anywa
maeneo hayo.
Rais Dkt. Magufuli pia amewataka Wakuu wa Mikoa kushughulikia
migogoro ya wakulima na wafugaji na kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa juhudi
na maarifa na kuzalisha chakula cha kutosha katika maeneo yao.
Katika kikao hicho Wakuu wa Mikoa
wamempongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuwapigania Watanzania hasa
wanyonge na wamemuhakikishia kuwa wataendelea kumuunga mkono katika juhudi hizo
ikiwemo kudhibiti wizi wa rasilimali za Taifa kama vile madini na maeneo ya
hifadhi za wanyamapori.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment