Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akielekezwa jinsi ya kujaza fomu za kununua hisa za Vodacom Tanzania PLC na Mkurugenzi wa wakala
wa hisa wa Orbit Securities,Gerase Kamugisha (kushoto) wakati alipokuwa akinunua hisa zake
na mke wake Mary Majaliwa(hayupo pichani)zenye thamani ya shilingi milioni 20
katika hafla fupi iliyofanyika ofisini
kwake jijini Dar es Salaam leo.Wanaoshuhudia
kutoka kushoto ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwekezaji,Bi.Beng’i Issa na Mkurugenzi mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC,Ian Ferrao.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania,
Kassim Majaliwa akikabidhiwa fomu ya kununua hisa za Vodacom Tanzania PLC na
Mkurugenzi wa wakala wa hisa wa Orbit Securities ,Gerase Kamugisha wakati wa hafla fupi ya kununua hisa zake na
mke wake,Mary Majaliwa(hayupo pichani) zenye thamani ya shilingi Milioni 20.Hafla
hiyo ilifanyika ofisini kwake jijini Dar
es Salaam leo,Anaeshuhudia kulia ni Mkurugenzi
Mkuu wa Vodacom Tanzania PLC,Ian Ferrao.
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amenunua hisa za kampuni ya Vodacom Tanzania Plc zenye thamani ya sh.
milioni 10 pamoja na nyingine za sh. milioni 10 kwa ajili ya mke wake, Mary
Majaliwa.
Waziri Mkuu amechukua
hatua hiyo leo hii (Ijumaa, Mei 5, 2017) wakati akizungumza na waandishi wa
habari mbele ya wakuu wa Masoko ya Hisa na Dhamana; Soko la Hisa la Dar es Salaam,
viongozi wa Baraza la Uwezeshaji na kampuni ya Vodacom katika ukumbi wa Ofisi
ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu
amewasihi Watanzania walioko ndani na nje ya nchi wachangamkie fursa ya kununua
hisa hizo ili waweze kuwa wamiliki wa kampuni kupitia hisa zao. “Hii ni fursa
kwa Watanzania kumiliki kampuni. Ukinunua hisa, unashiriki kikamilifu kumiliki
kampuni na pia unaboresha uchumi wako binafsi. Ninawasihi Watanzania wote tumieni
fursa hii kununua hisa hizo kabla muda haujaisha,” alisisitiza.
Alisema watumishi
wa umma wamepewa ya kununua hisa hizo kupitia mipango iliyowekwa na Makatibu
Wakuu wao lakini pia amewasihi viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi wachangamkie
fursa hiyo ili nchi iweze kupata kodi kupitia makampuni hayo.
“Hii ni fursa
kwa kila Mtanzania, kwa viongozi kwa taasisi na mashirika ya umma, taasisi
binafsi, wajasiriamali wadogo kama akinamama lishe au madereva wa bodaboda. Watanzania
walioko nje ya nchi (Diaspora) nao pia wanunue hisa kwani watakuwa wanachangia
uchumi wa nchi na wakati huo wanaweka akiba nyumbani,” aliongeza.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira hiyo, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango uwekezaji kwenye hisa ni njia mojawapo ya
kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa nchi.
“Huko mtaani
ukisema uchumi wa nchi unakua, watu wanabisha wakidai kuwa hawaoni unakua kwa
sababu hawana fedha mifukoni. Hii ni fursa nyingine ya kuwawezesha kukua
kiuchumi, ninaomba waichangamkie,” alisema.
Alisema sekta
ya mawasiliano ni miongoni mwa sekta inayokua kwa kasi hapa nchini kwani katika
robo tatu ya mwaka, sekta hiyo imekua kwa asilimia 11.3. “Niwasihi Watanzania wenzangu,
tununue hisa za Vodacom ili tuweze kuboresha uchumi wetu,” alisema.
Alisema anatoa
ombi maalum kwa wafugaji kukubali kuuza mifugo yao na kununua hisa ili
kupunguza idadi ya mifugo yao, jambo ambalo alisema litapunguza migogoro baina yao
na wakulima.
“Wakulima wa
vitunguu, alizeti, maua au wafugaji wa samaki nao pia wanaweza kununua hisa na
kuwa na mitaji kwa ajili ya shughuli zao. Ninawasihi wote watumie fursa hii ili
kumiliki kampuni,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Soko
la Mitaji na Dhamana, Bi. Nassama Masinda alisema amefurahishwa kuona Waziri Mkuu
akinunua hisa za kampuni ya Vodacom katika soko la awali.
Alisema uuzwaji wa hisa hizo ni utekelezaji wa Sheria
ya Fedha ya mwaka 2016 kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kuwa wamiliki wa makampuni
ya simu za mikononi hapa nchini. “Marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya
Kielektroniki na Posta sura ya 306 yanazitaka kampuni za simu na mawasiliano ya
kielektroniki kuuza si chini ya asilimia 25 ya hisa zao kwa umma wa Tanzania
kupitia masoko ya mitaji (IPO).”
Alisema baada ya hapo hisa hizo zinapaswa kuorodheshwa
kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya kukidhi matakwa ya Sheria ya
Masoko ya Mitaji na Dhamana, sura ya 79. Kampuni ya Vodacom ilitoa hisa milioni
560 kwa umma kwa bei ya sh. 850 kila moja na hivyo kutarajia kukusanya sh.
bilioni 476.
Alisema hivi sasa, wawekezaji kwenye masoko ya mitaji
ni watu 500,000 tu ikilinganishwa na Kenya ambayo ina wawekezaji milioni 1.7;
Uganda (40,000) na Rwanda (14,000). “Vodacom ina wateja milioni 6.2, iwapo nusu
ya wateja wake wote watashiriki ununuzi wa hisa, idadi ya wawekezaji kupitia
masoko ya mitaji na dhamana itaongezeka kwa asilimia 1,140. Na haya yatakuwa ni
mageuzi makubwa katika sekta ya masoko ya mitaji si hapa nchini tu bali katika Afrika
Mashariki,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Dodacom, Bw. Ian Ferrao alisema mauzo
ya hisa yanayofanywa na kampuni hiyo ni makubwa mara nne ya mauzo ambayo
yamewahi kufanyika hapa nchini.
Alisema kampuni hiyo ambayo imekwishafanya kazi kwa
miaka 17 hapa nchini, imewekeza zaidi ya sh. trilioni mbili katika mtandao wa
mawasiliano nchini Tanzania.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment