Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Sunday 30 April 2017

MPIGAPICHA WA TSN MOHAMED MAMBO ATWAA TUZO YA MPIGAPICHA BORA EJAT 2016

Mpigapicha Mkuu wa Magazeti ya Daily News, Habarileo na Spotileo, Mohamed Mambo akikabidhiwa tuzo ya EJAT baada ya Kuibuka Mpigapicha Bora wa EJAT 2017. Mambo alikabidhiwa tuzo hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Zamani wa Magazeti ya The Guardian Ltd ambaye pia ni Mkufunzio wa Uandishi wa Habari nchini, Kiondo Mshana katika Hafla ya kukabidhi tuzo hizo jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam.
**************
Na Katuma Masamba

MPIGA Picha wa Magazeti ya Serikali (TSN), Mohammed Mambo ameibuka mshindi wa tuzo ya mpigapicha bora, huku mwandishi wa gazeti la Habarileo Shadrack Sagati akiibuka mshindi wa pili katika kipengele cha uandishi wa habari za data katika Tuzo za Umahiri wa uandishi wa Habari (EJAT) mwaka 2016.


Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika jijini Dar es Salaam na ilihusisha vipengele 19 vilivyoshindaniwa na waandishi kutoka kwenye magazeti, radio na televisheni. Jumla ya waandishi 66 waliteuliwa kuwania tuzo hizo zinazoendeshwa na Baraza la Habari (MCT).


Washindi wa tuzo za mwaka huu waliteuliwa na majaji mbalimbali ambao ni Ndimbara Tegambwage, Hassan Mhelela, Pili Mtambalike, Dk Mzuri Issa Ali, Mwanzo Milinga, Nathan Mpangala na Dk Joyce Bazira ambaye alikuwa katibu wa jopo na Valeria Msoka ambaye alikuwa kiongozi wa jopo hilo la majaji.


Kazi zilizowasilishwa MCT kwa ajili ya kushindanishwa zilikuwa zaidi ya  810, zikiwemo zaidi ya 435 kutoka vyombo vya habari vya kielektorini na kazi zaidi ya 374 kutoka kwenye magazeti. Kazi hizo ni nyingi ikilinganisha na zile za mwaka 2015 ambako jumla ya kazi zilikuwa 568. Mshindi wa jumla wa tuzo hiyo kwa mwaka huu ni Florence Majani kutoka gazeti la Mwananchi.


Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo hizo, Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Jenerali Ulimwengu ambaye pia ni mwandishi mkongwe licha ya kuwapongeza washindi aliwataka waandishi ambao hawakufanikiwa kupata tuzo kuongeza juhudi katika kazi zao.


"Nashauri mkadurufu kazi za washindi, mkaone mlijikwaa wapi na kipindi kingine mtafanya vizuri zaidi," alisema mwandishi huyo mkongwe ambaye alitumia hotuba yake kama kuwafunda waandishi wa habari.


Alisema tasnia ya habari si ya watu walioshindwa masomo na kuikimbilia wakidhani ni nyepesi, bali ni taaluma inayohitaji watu mahiri na makini ambao wamejitolea kufanya mambo yasiyowahusu.


Alisema tasnia ya habari ni muhimu katika maisha ya binadamu kwa sababu inatoa nafasi kwa wanajamii kuungana, kuwasiliana na kubadilishana mawazo ili kuondoa tofauti miongoni mwao kupitia vyombo vya habari.


“… Uandishi wa habari ni shughuli yenye uwerevu na umakini wa hali ya juu wa kujua kitu na matokeo ambayo wanajamii hawana nia, hawajui na hawafahamu. Kuna muda huwa nasema mwandishi wa habari ni yule mtu anayeejiingiza katika mambo ambayo binafsi hayamuhusu, bali yanaigusa jamii,” alisema Ulimwengu.


Ulimwengu aliwataka wanahabari kujituma na kuwa makini katika uandaaji wa habari na kutambua kuwa wanaofanyia kazi baadhi yao wanajua kuliko wao na pia  kutotumia kigezo cha kuwa katika tasnia hiyo kudhani wanajua kuliko wao.


Aidha, alitoa mwito kwa wanahabari nchini kujenga utamaduni wa kujiendeleza kielimu, lakini pia kuwa kujenga tabia ya kusoma mara kwa mara vitabu na majarida, kusikiliza na kujifunza mambo mbalimbali ili waweze kufanikiwa na kutekeleza kazi zao kwa ufanisi.


Alisema mwandishi wa habari asiyependa kusoma vitabu na kujifunza kila wakati hawezi kuwa mahiri na wala kazi zake haziwezi kuwa nzuri.


“Kitabu ni rafiki mkubwa sana kwa wanahabari na hiyo ni silaha, waandishi tunatakiwa kusoma, kusikiliza na kujifunza kwa wenzetu waliofanikiwa. Chukulieni kazi mnayoifanya kuwa ni shughuli muhimu na inayohitaji umakini wa hali ya juu kwani utoa matokeo na kuhabarisha mambo ambayo wananchi hawajui na hawafahamu,” alisema.


Ulimwengu pia alishauri serikali kulinda usalama wa wanahabari kwani hivi karibuni kumeokea matukio ya wanahabari kupigwa na kunyanyaswa wakati wakitekeleza kazi zao.


Aidha, Aliwataka waandishi kuhakikisha wanaweka kumbukumbu sahihi za wanausalama na askari polisi waliowashambulia na baadae kuwadai fedha nyingi kama fidia ya matukio mabaya waliyowafanyia.


“Waandishi mkishambuliwa na hao watu nendeni mahakamani na ukishindwa kata rufaa na huko ndio utaenda kudai fidia kwa kitendo walichokifanyia,” alisema.



Baadhi ya vipengele hivyo ni mwandishi bora wa habari za uchumi, biashara na fedha, habari za michezo na utamaduni, habari za afya, Kilimo, Elimu, habari za uchambuzi wa matukio, habari za utalii.


Vingine ni mwandishi bora wa habari za Afya ya uzazi kwa vijana, habari za Ukusanyaji kodi, habari za uchunguzi, habari za takwimu, Mpiga picha bora, Mchoraji bora wa vibonzo, mpiga picha bora wa televisheni.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment