MABAO mawili ya Mbwana Samatta yameiwezesha timu ya Taifa ya Tanzania kuibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya taifa ya Botswana hii leo.
Taifa Stars wakicheza nyumbani katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki ndani ya dimba la Uwanja wa Taifa na kushuhudiwa na mashabiki wachache walioongozwa na Waziri Mpya wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe na Mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye walianza kupata bao kunako dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa Nahodha wake anaecheza soka la kimataifa huko Ubelgiji na timu ya K.R.C Genk, Mbwana Samatta.
Stars ikicheza kufa na kupona kujinusuru na vichapo vya mara kwa mara ilipata bao lake la pili dakika ya 87 kupitia tena kwa Mbwana Samatta kutokana na mpira wa adhabu ndogo iliyopigwa nje ya kumi na nane baada ya yeye kufanyiwa madhambi.
Mkwaju huo wa Samatta uliopigwa kiufundi ulipenya ngome ya Botswana na kumshinda Mlinda Mlango wa timu ya Taifa ya Botswana akilamba nyasi huku mpira ukitinga wavuni na kutingisha nyavu.
Mchezo huo umeweka rekodi nzuri kwa kocha mzawa aliyekabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo, Salum Mayanga lakini pia ni rekodi nzuri kwa Waziri mpya wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe aliyechukua mikoba ya Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye aliyeiongoza Wizara hiyo kwa mwaka mmoja.
Waziri
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe
(wapili kushoto) akifurahia matokeo ya Taifa Stars na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye , kushoto ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamali Malinzi, kulia anaeonekana kidogo ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo, Yusuf Singo Omar.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment