Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisoma Bungeni hotuba ya Bajeti ya Ofisi yake leo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma
kwa watu wenye ulemavu kwa kuzingatia sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na kusimamia
uundwaji wa kamati zinazoshughulikia masuala yao hapa nchini.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) wakati akiwasilisha hotuba
ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi
ya fedha za ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Bungeni dodoma.
Amesema Serikali itaboresha mazingira ya watu wenye ulemavu kwa
kuhakikisha uundwaji wa kamati zao zinazotambulika kisheria ili kusaidia
kutatua changamoto zinazowakabili na kuhakikisha kila mkoa unaunda kamati hizo
ambapo hadi sasa mikoa 12 imekamilisha zoezi la uundwaji wa kamati hizo.
“Tayari Serikali imeunda kamati za watu wenye ulemavu katika mikoa 12 ya
Geita, Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Njombe, Pwani, Singida, Rukwa,
Shinyanga, Simiyu na Tabora. Ufuatiliaji unaendelea kufanyika ili kuhakikisha
kuwa mikoa mingine nayo inaunda kamati hizo,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha uboreshaji wa huduma kwa watu
wenye ulemavu, Serikali imeendelea kutoa vifaa zaidi ili waweze kushiriki
katika shughuli za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanajikwamua
kiuchumi.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa vifaa saidizi kwa
jamii ya watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kufanya shughuli zao bila utegemezi
kwa kuwapatia baadhi ya vifaa ikiwemo viti mwendo 240, bajaji 6, magongo ya
kutembelea 350, kofia pana 128, fimbo nyeupe 175, miwani maalum kwa wenye uoni
hafifu 70, shime sikio 20, vyerehani 8, vifaa vya kukuzia maandishi 65, mafuta
maalum ya kukinga ngozi dhidi ya mionzi ya jua 35, viti maalum vya kuogea 50 na
nyenzo nyingine za kujimudu,” alisema.
Alisema Serikali imeendelea kuviboresha vyuo vya watu wenye ulemavu vya
Yombo, Dar es Salaam na Sabasaba, Singida ili kuhakikisha wanashiriki katika
fursa zote ikiwemo za elimu ili wawe na ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika
fursa za ajira nchini ikiwa ni utekelezaji wa Sheria Na. 9 ya Watu Wenye
Ulemavu ya mwaka 2010.
Alisema Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni
pamoja na kukamilisha uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Maendeleo wa Watu wenye
Ulemavu, kuanzisha madawati ya watu wenye ulemavu, kuhamasisha sekta binafsi na
umma kuweka miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu na kuwataka waajiri wote wawaajiri
watu wenye ulemavu wenye sifa kwenye nafasi mbalimbali.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment