Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wapili kulia)
akizundua huduma ya 4G LTE za kampuni ya Simu ya Tanzania (TTCL) mkoani Dodoma
jana. Kutoka kulia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof Makame Mbarawa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri
Kindamba.
Na
Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi zote za Umma ambazo zinadaiwa na
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kuhakikisha zinalipa madeni yao kabla ya Juni
30, 2017.
Waziri
Mkuu ametoa rai hiyo leo, Mjini Dodoma katika viwanja vya Bunge wakati wa
uzinduzi wa huduma ya 4G LTE za kampuni hiyo ya simu kwa Mkoa wa Dodoma.
“Kuhusu
shilingi Bil. 11.5 ambazo TTCL inazidai Taasisi mbalimbali za Umma, Mheshimiwa
Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, kaa na wadaiwa sugu wote, thibitisheni
madeni husika kisha mkubaliane namna ya kulipa madeni hayo. Nijuavyo kila
Wizara inatenga bajeti kwa ajili ya ankara za simu, sasa hayo malimbikizo
yanatoka wapi?” alisema Kassim Majaliwa.
Aidha
amezitaka Taasisi hizo zinazodaiwa na TTCL kuhakikisha zinakamilisha madeni yao
kabla ya kufikia Juni 30, 2017 ili kampuni hiyo iweze kufanya kazi ipasavyo na kuendana
na ushindani wa kibiashara uliopo.
Pia,
ameitaka kampuni hiyo kujifunza kutoka kwenye makampuni binafsi namna yanavyoendeshwa
na kuiga baadhi ya mbinu zao, hususan katika kupunguza gharama za uendeshaji.
Kassim
Majaliwa amesema kwamba, Serikali ina matarajio makubwa kutoka katika kampuni
hiyo kutokana na kuwa na imani kwamba kampuni hiyo ina maarifa ya kujifunza
kutoka kwa waliofanikiwa kwenye sekta hiyo.
Vile
vile ameitaka kampuni hiyo kujifunza kutoka katika mashirika ya Umma ya Simu
kwenye nchi nyingine ambayo yanajiendesha kwa faida, kwa kuiga mbinu ambazo
wanazitumia na kuziweka katika muktadha wa nchi ya Tanzania.
Waziri
Mkuu amempongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
pamoja na timu yake kwa hatua ambayo kampuni hiyo imefikia. Aidha amemtaka
Waziri huyo kufuatilia kwa karibu kampuni hiyo ili iweze kutoa ushindani wa
kutosha kibiashara, ijiendeshe kwa faida, itoe gawiwo stahiki kwa Serikali,
ilipe kodi na zaidi ya yote fedha za Umma zilizowekezwa ziweze kutumika vizuri.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment