Na
Ramadhani Juma,Ofisi ya Mkurugenzi
HALMASHAURI
ya Manispaa ya Dodoma imeishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kuipatia
fedha kwa ajili ya kuimarisha Miundombinu ya Shule mbalimbali za Manispaa hiyo
chini ya mradi wa ‘Lipa kwa Matokeo’ maarufu kama ‘P4R’.
Shukrani hizo zimetolewa na
Afisa Elimu ya Msingi wa Manispaa ya Dodoma Mwisungi Kigosi alipotembelea Shule
mbili za Nkuhungu na Chango’mbe ambazo kila moja inajengewa madarasa mapya nane
kwa fedha za mradi huo.
Kwa mujibu wa Kigosi, mradi
huo pamoja na mambo mengine, unajenga miundombinu mbalimbali katika Shule sita
za Msingi ambapo jumla ya Shilingi milioni 993.1 zinatekeleza kazi hizo.
“Fedha za P4R zina kazi
nyingi kama vile kusaidia kukusanya takwimu
mbalimbali, kuhamisha Walimu kwa mujibu wa Ikama, na kubwa kabisa ni kujenga
miundombinu kama madarasa mapya, kukarabati madarasa ya zamani, na kujenga
Vyoo” Alifafanua.
Alisema mradi huo umekuwa
mkombozi kwa Shule husika kwa kuongeza na kuimarisha miundombinu kama madarasa
kutokana na idadi kubwa ya Wanafunzi inayopelekea upungufu wa madarasa katika
baadhi ya Shule.
“Kwa mfano Shule ya Msingi
Nkuhungu, mwaka huu wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la kwanza ni mia
sita…kwa hiyo utaona ni jinsi gani madarasa yanahitajika na hii inatokana na
Kata hiyo kuwa na Shule moja tu ya
Serikali” alisema Kigosi.
Aidha, alizitaja Shule
nyingine nne ambako mradi huo unatekelezwa kuwa ni Mahomanyika, Mwenge, Ihumwa,
na Nzasa, na kwamba Fedha hizo zimepatikana baada ya Manispaa kukidhi vigezo ikiwemo
kuwa na takwimu za uhakika za masuala ya Elimu.Baadhi ya Wanafunzi wa Shule
zilizopata Fedha za mradi huo wamepongeza juhudi za Serikali katika kuwatatulia
chang’amoto hususani za miundombinu kama vyumba vya Madarasa na Vyoo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment