JENGO la kampuni ya Mawakili
wa IMMA lililopo Upanga jijini
Dar es Salaam limevamiwa usiku wa kuamkia leo na kulipuliwa kwa kitu chenye
kishindo kikubwa kinachodhaniwa kuwa ni
bomu jambo lililosababisha uharibifu mkubwa
huku kukiwa hakuna kilichochukuliwa. Anaandika Katuma Masamba picha na Mroki Mroki.
Mlipuko huo unadaiwa kutokea majira ya saa 7:30 usiku wa
kuamkia jana, na walinzi wawili wa kampuni ya Knight Support iliyokuwa ikilinda
jengo hilo wakiokotwa eneo la Kawe
wakiwa hawajitambui.
TSN Digital ilifika eneo la tukio na kuona uharibifu
uliosababishwa na mlipuko huo katika jengo la Mawakili hao na jengo la ghorofa
nne la Reliance House pamoja na nyumba ya makazi ya Mohammed Ismail.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya IMMA yenye mawakili 25, Sadock
Magai amesema jengo lao lilitaka
kuungua, lakini limeharibiwa ila bado
hawajajua sababu ya watu waliofanya hivyo.
Mbali na Magai Wakurugenzi wenza wanaunda IMMMA ADVOCATES ni pamoja na
Protase Ishengoma, Fatma Karume, Faustin Malongo, Gaspar Nyika, Samah Salah na Madina Chenge.
Amesema uharibifu uliotokea ni mkubwa, ila wakiwa kama
Mawakili wenye taaluma hawataki kuhisi sababu za mlipuko huo bali wanasubiri
uchunguzi wa Polisi ndio uweze kubaini.
Naye Kaimu Kamanda
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu
Dar es Salaam, Lucas Mkondya, amesema
Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kuweza kubaini aina ya mlipuko na
sababu haswa za kutokea kwa tukio hilo.
Amewataka wananchi na hata wafanyakazi wa jengo hilo kuwa wavumilivu na kusubiri ripoti ya
jeshi hilo kwani askari wako eneo la tukio wakiendelea na uchunguzi.
Wafanyakazi wakitoka ndani ya jengo hilo.
Mwandishi wa kujitegemea akipita nje ya jengo hilo.
Miongoni mwa uharibufu mkubwa uliofanywa na mlipuko huo ni kama huu
Baadhi ya maeneo yalifukuliwa kuonesha kuwa milipuko ilitegwa ardhini kuteketeza jengo hilo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment