WAFANYAKAZI
wa kampuni ya LABA Construction Ltd ambao ni vibarua wa kampuni ya Sumitomo Mitsui
Construction company Ltd inayojenga barabara ya juu (Flyover) ya Tazara
wamegoma wakishinikiza kuongezwa maslahi yao pamoja na kuitaka kampuni ya Laba
kuondoka. Anaandika Katma Masamba.
Wafanyakazi
hao walianza mgomo kuanzia siku ya jana ambapo wanaitaka kampu ni ya Laba ambayo
wanadai inafanya kazi ya udalali kuondoka kwa kuwa ndio inawanyonya kwani
kampuni ya Sumitomo imekuwa ikilipa Sh 37,000 kwa fundi na kibarua Sh 25,000
lakini kampuni hiyo imekuwa ikilipa Sh 14,000 kwa fundi na Sh 10,000 kwa
kibarua.
Akizungumza
kwa niaba ya wenzake mmoja wa wafanyakazi hao Jackson Mselemu amesema,
wanachodai ni kutaka kuongezewa maslahi na kwamba wanataka yalipwe moja kwa
moja bila kuwepo mtu wa kati ambayo ni kampuni ya LABA.
"Hii
kampuni ya LABA ndio inatudhulumu , tunakatwa hela za PPF lakini tumeenda
kuuliza tunaambiwa hakuna hela iliyowahi kupelekwa kuele, kwa hiyo sisi
tunaomba mtusaidie, lakini pia hatutaki fedha zetu zilipwe kupitia Tigo Pesa,
tulipwe kwa njia ya benki," amesema Mselemu.
Naye
Hussein Bakari amesema, kwenye mfuko wa PPF wameambiwa kampuni ya LABA
haitambuliki hivyo ni vyema wakarudi kwa mwajiri wao ili wapate ufafanuzi
mzuri, lakini hakuna pesa yoyote
iliyopelekwa kwa ajili yao.
Mashaka
Nyerere amesema, hawajagomea kazi bali wanachokigomea ni maslahi kwa kuwa
malipo wanayoyapata hayaendani na kazi wanazofanya.
Alisema kazi wanazofanya ni
ngumu na zinafanywa katika maeneo ya hatari, lakini maslahi wanayopokea ni
mabovu.
"Sisi
tuko tayari kufanya kazi lakini tunataka hii kampuni ya udalali ya LABA iondoke
tuko tayari kufanya kazi tukalipwa hata Shilingi elfu kumi na Mjapani,
kwasababu tunajua tutambana wapi kuliko huyu mswahili," amesema Nyerere.
Kwa
mujibu wa mkataba baina ya kampuni ya LABA na mfanyakazi unaonesha malipo ya
kazi kwa saa ni Sh 1,250, kwa siku Sh 10,000, malipo baada ya muda wa kazi
kuisha Sh 1,875 kwa saa na siku ya jumapili na sikukuu Sh 2,500 kwa saa huku
ikiwa na sehemu ya kujaza namba ya simu iliyosajiliwa na Tigo Pesa.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment