JESHI la Polisi Tanzania limetoa tahadhari kwa
wananchi juu ya utapeli unaofanywa na kundi la watu wanaolaghai watu na
kujipatia fedha kwa minajili ya kuwasaidia kujiunga na jeshi hilo. Anaandika Mroki Mroki.
Taarifa iliyo tolewa na Jeshi la Polisi kupitia kwa Msemaji wa wake, Naibu Kamishna
(ACP), Advera Bulimba (pichani) ilisema kikundi kidogo cha matapeli wanazunguka katika maeneo
mbalimbali hususani vijijini na kuwalaghai vijana kwamba wao ni watumishi ama
waajiriwa wa Jeshi la Polisi na kujipatia fedha.
Alisema watu hao wamekuwa wakitapeli fedha hizo kutoka kwa wananchi hasa vijana
kwa udanganyifu kwamba watawapatia ajira ndani ya Jeshi la Polisi jambo ambalo
siyo la kweli.
“Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa wananchi kwamba ndani ya Jeshi la Polisi
hakuna ajira zilizotangazwa, na hivyo tunawataka wananchi wote kuwa makini na mtandao
huo wa matapeli,”ilisema taarifa hiyo ya ACP Bulimba.
Taarifa hiyo ilisema kuwa mfumo wa ajira ndani ya Jeshi
la Polisi ni wa wazi na una utaratibu maalum ambao hutangazwa kwa wananchi kwa mujibu
wa taratibu za Jeshi la Polisi.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi
linatoa onyo kali kwa wote wenye tabia hiyo ya utapeli kuacha mara moja na endapo
mtu yeyote atabainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha Polisi linatoa rai kwa wananchi wote wenye taarifa za matapeli hao kuzifikisha
haraka katika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu ili sheria iweze
kuchukua mkondo wake.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment