Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameagiza
kufanyika kwa uhakiki wa hati za hakimiliki zote zilizotolewa kwenye ardhi oevu
na kuzibatilisha haraka iwezekanavyo ili kuokoa ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha
Mkuu.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo
hilo mjini Dodoma wakati wa kupokea Taarifa ya Kikosi Kazi cha Kitaifa cha
Kuokoa Mifumo wa Ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu kilichoundwa na Ofisi yake
ili kukoa uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea katika Bonde la Mto Ruaha
Mkuu.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia ameagiza watendaji wa ofisi yake
ushirikiane na Tamisemi wahakikishe wanawaondoa watu wote waliovamia maeneo ya
hifadhi ya bonde hilo mara baada ya kumaliza kuvuna mazao yao.
Amesema
hatua hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kurejesha hali ya uoto wa asili ulioharibiwa
kwa kiasi kikubwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa sheria zote zinazohusiana na
usimamizi endelevu wa ikolojia na mazingira ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu ikiwemo
sheria ya mazingira na nyingine zitekelezwe kwa ukamilifu na kila mhusika.
Amesema
kuwa ili kutekeleza maagizo hayo ni vyema wadau wote wa mazingira washirikiane
kikamilifu na kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika ili wajione nao ni
sehemu ya mkakati wa kuokoa mfumo wa ikolojia wa bonde hilo kwa ajili ya ustawi
wa maisha yao na maslahi ya Taifa kwa ujumla.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
January Makamba amesema kikosi kazi hicho ambacho kilizinduliwa rasmi na Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan tarehe 11 April 2017 mjini Iringa kimefanya
kazi kubwa kwa siku 30.
Amesema
unauhakika taarifa ya kikosi kazi hicho ikifanyiwa kazi ipasavyo italeta
mabadiliko makubwa katika Uhifadhi wa Ikolojia katika Bonde la Mto Ruaha Mkuu na
kurejesha hali yake ya awali.
Waziri
Makamba amesema kazi kama hiyo itafanyika katika maeneo mbalimbali nchi ili
kuhakikisha uharibifu kwenye mabonde yote nchini inakomeshwa.
Ameeleza
kuwa jitihada hizo zilizochukuliwa na ofisi yake tayari zimewavutia baadhi ya
wahisani ambao tayari wameonyesha nia ya kushirikiana na Serikali katika
Uhifadhi wa mazingira nchini.
Baadhi
ya Mawaziri ambao wamepewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo watatekeleza
haraka iwezekanavyo maelekezo ya Makamu wa Rais ili kukomesha uharibifu mkubwa
wa mazingira katika Bonde la Mto Ruaha Mkuu.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment