Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Sunday 12 March 2017

RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA SIR GEORGE KAHAMA



 Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mmoja wa Waasisi wa Taifa na Waziri Mstaafu, Sir George Kahama kufuatia kifo cha kiongozi huyo kilichotokea leo tarehe 12 Machi, 2017.

Sir George Kahama amefariki dunia akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika Salamu zake Rais Magufuli amesema Taifa limempoteza mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru, maendeleo na ustawi wa jamii ya watanzania akiwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi hususani kuwa miongoni mwa Mawaziri katika Baraza la kwanza la Mawaziri ambapo alishika wadhifa huo kwa awamu tatu za uongozi wa Tanzania.

“Sir George Kahama alikuwa kiongozi shupavu, mzalendo, mwanasiasa mahiri, aliyewapenda Watanzania na aliyejitoa kushirikiana na viongozi wenzake akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kupigania uhuru, kujenga misingi ya Taifa likiwemo Azimio la Arusha, kujenga misingi ya uchumi wa ujamaa na kujitegemea na mengine mengi, kwa hakika hatutamsahau”

“Japo kuwa Sir. George Kahama ametangulia mbele za haki, sisi viongozi tuliopo tutamuenzi kwa kuhakikisha tunaendeleza juhudi za kuipigania Tanzania aliyoshiriki kuijenga, na pia tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli katika salamu hizo.

Pamoja na familia ya Marehemu Sir. George Kahama, Mhe. Dkt. Magufuli amewapa pole nyingi wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wabunge, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huo.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment