Na Hamisi Kibari, Simiyu
MKOA
wa Simiyu umedhamiria mwaka huu kuanza kujenga kiwanda cha aina yake Afrika
Mashariki cha kutengeneza bidhaa za afya zinazotokana na pamba baada ya hatua
za upembuzi yakinifu kuelekea kukamilika na michoro ya ramani ya kiwanda
kuthibitishwa.
Akiongea
jana, siku moja kabla ya Jukwaa la biashara kufanyika mkoani hapa leo, Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema hatua hiyo, siyo tu kwamba inalenga kutekeleza
mpango wa kujenga Tanzania ya viwanda, lakini pia itasaidia katika kuongezea
thamani ya zao la pamba. Mkoa wa Simiyu ndio unaotoa asilimia 60 ya pamba yote inayolimwa
Tanzania kwa mujibu wa takwimu za mwaka huu.
“Simiyu
tunaongoza kwa kuzalisha pamba nchini, lakini unajiuliza tuna sababu gani ya
hii nchi kuagiza pamba za kusafisha masikio, tuna sababu gani ya kuagiza
bandeji, kuagiza pampasi, kuagiza taulo za usafi wa akina mama, tuna sababu
gani ya kuagiza pamba za kusafishia vidonda? Hatuna sababu hiyo,” alisema.
Alisema
walikaa na kuona ili wazo la kuanzisha kiwanda hicho kitakachogharimu takribani
Sh bilioni 250 lisibaki nadharia wakaamua kushirikisha wadau na sasa linaelekea
kuwa kitu halisi.
Mtaka aliyasema hayo wakati akielezea maandalizi ya Jukwaa la Biashara linalofanyika kesho Februari 13,2017 lililoandaliwa na TSN, wachapishaji wa magazeti ya HabariLeo na Daily News, kwa
kushirikiana na Mkoa wa Simiyu, linawakutanisha pia wadau muhimu wa maendeleo
kama vile vyombo vya fedha; Benki za TIB na NMB, Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Kongamano hilo linatazamiwa
pia kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Simuyu kama taasisi
mbalimbali zinazoshughulika na biashara au uzalishaji wa bidhaa, masoko,
wabunge, halmashauri, wenye viti wa mitaa, wafanyabiashara, wakulima,
wawakilishi wa waendesha bodaboda, taasisi za kidini na kadhalika.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment