Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa Habari Mjini Dodoma leo kuhusiana kuanza kutumika kwa Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari 2016, na kanuni zake ya 2017.
Nimewaita hapa leo kwa lengo
la kuwapa taarifa rasmi wanataaluma ya habari na wananchi kwa ujumla kuhusu
mada iliyotajwa hapo juu. Kama mnavyofahamu, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alisaini Sheria ya Huduma za
Habari Novemba 16, 2016 na siku mbili baadaye yaani Novemba 18, 2016 Sheria
hiyo ikachapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Kwa mujibu wa kifungu cha 1
cha Sheria hiyo, ili ianze kutumika rasmi, Waziri wa Habari anatakiwa
kuitangaza tarehe ya kuanza kutumika. Napenda kuufahamisha umma kuwa nikiwa
Waziri mwenye dhamana hiyo nimeshatekeleza wajibu wangu kwa kutangaza kwenye
gazeti la Serikali kuwa sheria hii imeanza kutumika tangu Desemba 31, 2016
Ndugu wanahabari,
Kuanza kutumika kwa sheria hii
ni jambo muhimu sana kwa tasnia, kwa sababu sasa baada miaka mingi ya mijadala,
sasa tunaruhusa rasmi ya kuanza mchakato rasmi wa kuihamisha taaluma ya habari
kutoka fani ambayo mtu yeyote anaweza kujinasibu nayo, hadi kuwa taaluma kamili
yenye sifa mahsusi, maadili yanayojulikana lakini na vyombo vya kusaidia
kusimamia utekelezaji wake.
Kama tulivyosisitiza awali,
sheria hii pia inaleta mfumo madhubuti wa kulinda haki za wanahabari kukusanya,
kuhariri na kusambaza habari zao kwa uhuru. Vyombo vya habari sasa vitatekeleza
haki yao hii ya kikatiba bila vikwazo visivyokuwa na sababu.
Aidha, umma na wanatasnia ya
habari pia wanakumbushwa kwamba sheria hii, kwa lengo la kuwa na wanataaluma
wanaotekeleza vyema wajibu wao, na kama ilivyo kwa taaluma nyingine, imeweka
wajibu kwa wale watakaokiuka misingi na maadili ya taaluma. Hii ina maana
ukurasa mpya wa haki na wajibu umefunguliwa.
Katika utekelezaji wa sheria
hii kuna taasisi ambazo tayari zipo, zitaongezewa majukumu au kazi zake
kuhuishwa, kuna vyombo vipya vitaanzishwa na kuna taratibu mpya za kiutendaji
zitaandaliwa. Yote hayo Serikali itaendelea kutoa elimu na kuufahamisha umma
kadiri yanavyoendelea kukamilika.
Kanuni za Sheria ya Huduma za
Habari, 2017
Ndugu wanahabari,
Kwa mujibu wa kifungu cha 65
cha Sheria nikiwa Waziri wa Habari nimepewa jukumu la kutunga kanuni za
kusaidia utekelezaji wa sheria hii. Napenda kwanza kuwashukuru wadau wengi
walioleta maoni yao tena kwa kujenga hoja
kwa maandishi na utafiti. Ninayofuraha leo kuwataarifa kuwa tumefaidika
sana na maoni hayo na kanuni hizo sasa zimeshachapishwa kwenye Gazeti la
Serikali la Ijumaa Februari 3, 2017.
Kanuni hizi zimesheheni
masuala ya kusaidia utekelezaji wa sheria na hasa muktadha mzima wa kufikia
Tanzania kuwa na kile nilichokiainisha hapo juu-vyombo vya habari vyenye uhuru
wa kutosha lakini pia vinavyowajibika ipasavyo kwa umma.
Kubwa katika kanuni hizi na
ambalo limetolewa maoni na wengi wakati wa kukusanya maoni ya wadau, nafahamu
wengi pia mnahamu sana ya kulisikia, ni kiwango cha elimu ili mtu aweze
kuruhusiwa kufanyakazi ya taaluma ya habari nchini.
Tumesoma, tumechambua maoni ya
wengi; wapo waliotaka iwe cheti, wengine diploma, wengine digrii wengine
walitaka iwe hata PhD na wapo waliotaka iwe mtu yeyote anayejua tu kusoma na
kuandika!Serikali imesimama katikati ya maoni hayo. Sifa ya chini kabisa kwa
kuanzia itakuwa ni diploma ya uandishi wa habari.
Hata hivyo, Serikali imetoa
kipindi cha mpito cha miaka mitano kuanzia Januari mosi mwaka huu kwa waandishi
waliopo sasa na wanaotaka kuingia katika taaluma hii ambao hawana sifa hizi
wakasome.
Ili kusaidia wanahabari hasa
waliopo sasa kazini waweze kujiendeleza, kupitia Idara ya Habari MAELEZO,
tutaendelea kutoa press card bila kuwabana sana wanahabari kwa kuangalia vigezo
hivi vya kitaaluma bali dhamana ya waajiri wao tu.
Masuala mengine ya utekelezaji
wa sheria na kanuni hizi tutaendelea kuutaarifa umma kadiri yanayokamilika au
kuanza kutekelezwa. Tutaendelea pia kutoa elimu kwa umma.
Nawashukuru kwa kuniskiliza.
Nape M Nnauye
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment