Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka akizungumza na Waandishi wa Habri wa Magezeti ya Serikali (TSN) juu ya maandalizi ya Jukwaa la Biashara Simiyu linalotaraji kufanyika kesho mkoani hapa.
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Antony Mtaka akizungumza na ujumbe wa waandishi na maofisa wa Kampuni
ya Magezeti ya Serikali (TSN) kuhusiana na Jukaa la Biashara linalofanyika
mkoani humo leo na fursa mbalimbali zilizopo mkoani Simiyu. (Picha na Mroki
Mroki).
Na
Hamisi Kibari, Simuyu
“KESHO ni kesho Simiyu, asiye na mwana ataeleka
jiwe” labda ndio maneno ya Waswahili yanayoweza kueleza kwa kifupi hali
inayotazamiwa kujiri katika mkoa wa huo wa Kanda ya Ziwa kesho.
Ni ile siku iliyosubiriwa ya kuumulika kibiashara mkoa
wa Simiyu ulioanzishwa mwaka 2012, ambao umejipambanua kuwa ‘mkoa darasa’, mintarafu suala zima la ujenzi wa viwanda
nchini.
Mwezi uliopita, Rais John Magufuli alipotembelea mkoa
huu, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na mkoa chini ya mkuu wake, Anthony
Mtaka, katika kujenga uchumi wa viwanda na hivyo kuelekea kuifanya ndoto yake
ya Tanzania ya viwanda kutimia.
Kupitia Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN)
inayochapisha magazeti ya Daily News na HabariLeo pamoja na mitandao mbalimbali
ya kijamii, fursa za uchumi za mkoa huu darasa zitadadavuliwa na kuchambuliwa kesho,
na hivyo kuwasaidia wawekezaji wa ndani na nje kujua ‘kunani’ Simiyu.
Tayari timu kamambe ya TSN ikiongozwa na Mhariri Mtendaji,
Dk Jim Yonaz, imetia kambi Simiyu ili kukuletea kwenye macho yako na masikio
kwa nini Simuyu imejipambanua kuwa mkoa darasa wa viwanda.
Ukiwa na wilaya tano za Bariadi, Itilima, Maswa, Busega
na Meatu Simiyu ni mkoa ulioanza kutekeleza sera yake ya ‘wilaya moja, bidhaa
moja’ inayolenga kuifanya kila wilaya kuangalia raslimali zinazopatikana mahala
hapo na kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa zitokanazo na raslimali hiyo.
Kwa mfano, tayari wilaya ya Meatu imejipangia kuwa
gwiji la uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na maziwa nchini, wilaya ya Maswa
chaki, wilaya ya Busega inayopakana na Ziwa Victoria kuanzisha viwanda vya
samaki na kilimo cha umwagiliaji huku Bariadi ikijikita katika kuzalisha bidhaa
zitokanazo na zao la pamba.
Kwa usimamizi wa Mkuu wa Mkoa, Mtaka, tayari
viwanda vya maziwa na chaki vimeshaanza kazi na watu wanatumia bidhaa husika na
ajira nyingi zimezalishwa.
Katika kufanikisha shughuli ya kesho, TSN inashirikiana
na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki ya NMB, Benki za TIB Development na
TIB Corporate na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Kutokana na majukumu yake, taasisi hizo ni muhimu
katika kusaidia uwekezaji Simiyu kufanyika kwa urahisi na hivyo kuleta tija kwa
wana-Simiyu na nchi kwa ujumla.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment