Kamati
ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imefuta
adhabu dhidi ya wanafamilia wanne waliofungiwa kushiriki masuala la soka
kwa mwaka mmoja.
Wanafamilia
hao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Rukwa, James Mwakwinya; Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Blassy Kiondo; Kaimu Katibu wake, Ayoub
Nyaulingo pamoja na Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.
Haji
Manara alitiwa hatiani Aprili 23, mwaka huu kwa makosa ya lugha chafu
na za chuki kwa viongozi wa TFF na kupotosha umma dhidi ya kadi njano ya
mchezaji Mohammed Fakhi wa Kagera Sugar ambako alifungiwa kushiriki
masuala ya mpira kwa mwaka mmoja na faini ya Sh milioni tisa.
Viongozi
wa RUREFA walifungiwa kwa mwaka mmoja na faini ya Sh. milioni mbili kwa
kila mmoja kwa makosa ya kukiuka maagizo ya viongozi wa Kamati ya
Uchaguzi ya TFF iliyotaka wasitishe mchakato wa uchaguzi mkoa kwa kuwa
kulikuwa na rufaa iliyokatwa TFF.
Akizungumza
na Wanahabari leo Julai 17, 2017 Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya
TFF, Tarimba Abbas, alisema viongozi hao wamesamehewa adhabu zao kwa
kuwa waliomba kupitiwa upya kwa mashauri yao na kamati imeona ni bora
kuwaachia huru ili kuendeleza masuala ya soka.
“Wapo
wengi waliofungiwa wengine maisha na wengine adhabu fupi, msamaha huu
ni kwa wale ambao wameomba tu kupitiwa upya kwa adhabu zao, pia milango
ipo wazi kwa wengine ambao wanataka kupitiwa kwa mashauri yao, lakini si
kwa wale waliopanga matokeo uwanjani,” alisema Tarimba.
Kadhalika,
Tarimba aliwaomba viongozi wa TFF kuandaa semina ya Maofisa Habari na
Viongozi wa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ili kuepuka maneno
machafu ambayo yanasababisha wao kufungiwa.
“Inaonekana
viongozi na Maofisa Habari hawana maneno mazuri ya kuongea na wadau wa
soka na ndio maana matatizo ya kufungiwa yanajitokeza mara kwa mara,
naamini wakipata semina hiyo itawasaidia kujirekebisha na kupunguza kesi
kama hizo,” alisema Tarimba.
Kwa
niaba ya TFF, Ofisa Habari wa Shirikisho, Alfred Lucas, wameyapokea
mapendekezo hayo kutoka kwa Tarimba na kwamba tutafanyia kazi ili
kurekebisha makosa hayo kwa manufaa ya soka la Tanzania.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment