Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
katika mazungumzo na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Jasem Ibrahim Al Najem
alipofika kumtembelea Ikulu jijini Dar es salaam leo Juni 5, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akiangalia malori mawili ya kuzolea taka baada ya kumaliza mazungumzo na
Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Jasem Ibrahim Al Najem alipofika
kumtembelea na kukabidjhi msaada wa magari hayo Ikulu jijini Dar es
salaam leo Juni 5, 2017.
******************
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameishukuru
Serikali ya Kuwait kwa kutoa mkopo wa Dola za Marekani Milioni 51 sawa na takribani
Shilingi Bilioni 110 kwa ajili ya kujenga barabara ya Chaya - Nyahua Mkoani
Tabora yenye urefu wa kilometa 85 ambayo itaunganisha mawasiliano ya barabara
kati ya mkoa wa Singida na Tabora.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa shukrani hizo leo tarehe 05 Juni, 2017 Ikulu Jijini Dar es
Salaam alipofanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Ibrahim
Al Najem na kupokea msaada wa magari mawili ya kusombea taka ngumu yenye
thamani ya Dola za Marekani 200,000/- yaliyotolewa na Serikali ya Kuwait kwa
lengo la kuunga mkono kampeni ya usafi hapa nchini.
“Naomba
unifikishie salamu zangu kwa Mfalme wa Kuwait, mwambie tunathamini mchango
mkubwa wa Kuwait katika maendeleo ya nchi yetu, hizi fedha za barabara mlizotupatia
zitatusaidia kumalizia sehemu hiyo ya barabara ambayo ndio ilikuwa imebaki”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli pia ameishukuru Serikali ya Kuwait kwa kuunga mkono juhudi
mbalimbali za utoaji wa huduma za kijamii hapa nchini ikiwemo msaada wa Dola za
Marekani 250,000 kwa ajili ya kununulia vifaa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete navisima vya maji safi 27 vilivyochimbwa Jijini Dar es Salaam kwa ajili
ya wananfunzi na wananchi wa maeneo jirani na shule.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Kuwait kwa kutoa Dola za Marekani
Milioni 50 kwa ajili ya kuikarabati hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmoja iliyopo
Zanzibar.
Mhe.
Rais Magufuli pia ameiomba Serikali ya Kuwait kuweka alama ya kumbukumbu ya uhusiano
wake na Tanzania kwa kusaidia ujenzi wa barabara za Makao Makuu ya nchi Mjini
Dodoma na amemhakikishia Mfalme wa Kuwait Sheik Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na
ushirikiano kati ya Tanzania na Kuwait hususani katika masuala ya kiuchumi
ikiwemo mafuta na gesi ambayo imevumbuliwa kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.
Kwa
upande wake Balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Ibrahim Al- Najem ameelezea
kufurahishwa kwake na uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya nchi yake na Tanzania
na amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa Kuwait ipo tayari wakati wowote
kuunga mkono juhudi za maendeleo kulingana na vipaumbele vya Tanzania.
Wakati huo huo,
Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya
Nje wa Kongo Mhe. Leonard She Okitundu na kumhakikishia kuwa Tanzania inaunga
mkono juhudi za kumaliza tofauti kati ya pande zinazopinga nchini Kongo.
Pamoja
na kukabidhi barua yenye ujumbe wa Rais wa DRC Mhe. Joseph Kabila Kabange,
Balozi Leonard She Okitundu amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa hali ya Kongo ni
shwari na kwamba mchakato wa mazungumzo kati ya pande zinazopingana nchini humo
unaendelea vizuri.
Katika hatua nyingine,
Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya
Msumbiji ambaye ni Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Jenerali Atanasio Salvador
Ntumuke.
Baada
ya mazungumzo hayo, Jenerali Atanasio Salvador Ntumuke amesema Msumbiji
itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa mambo mbalimbali kwa kuwa nchi hizo ni
ndugu na zimesaidiana kwa mengi tangu harakati za kupigania uhuru ambapo
Tanzania ilitoa mchango mkubwa.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment