Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.

Have you got a good story?

Share your story, discuss the issues with Dailynews Blog.





Nafasi Ya Matangazo

Sunday 5 March 2017

RIPOTI YA UTAFITI WA VISABABISHI NA MADHARA YA NDOA ZA UTOTONI NCHINI, NEEMA KWA WANAWAKE WA KESHO

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Plan International mwaka 2016 lilifanya utafiti na kugundua kuwa nafasi ya watoto wa kike ulimwenguni haionekani machoni pa watu.

Hatua hiyo inatokana na sababu zinazoonesha kuwa takwimu zinazowahusu watoto wa kike ziko nyuma ya wakati, hazijakamilika na muda mwingine tafiti zake hazifanyiwi utekelezaji.

Nchini Tanzania imeonekana hakuna takwimu sahihi zinazoonyesha uhalisia wa changamoto anazozipata mtoto wa kike kutokana na ndoa za utotoni, hivyo kupelekea thamani ya mtoto wa kike kushuka katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo ambapo madhara yake yanaonekana baadae akiwa mtu mzima.

Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka Shirika la Plan International–Tanzania, Jane Mrema anasema kiwango cha ndoa za utotoni kwa Tanznia kimefikia asilimia 36 ambacho ni kiwango kikubwa zaidi ya kiwango cha Dunia ambacho ni asilimia 34 na kwa hesabu za kimkoa ni asilimia 59 kwa kila mkoa. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.

“Hiyo ndio sababu kubwa iliyopelekea Shirika letu kuungana na Serikali pamoja na mashirika mengine kufanya utafiti huo wenye lengo la kufahamu vitu vinavyopelekea ndoa za utotoni pamoja na madhara yake baada ya ndoa hizo kutokea,”anasema Bi. Jane.

Utafiti huo umefanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yakiwemo ya Shirika la kutetea haki za watoto (Plan International), Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Shirika linalohusiana na Utafiti na maendeleo ya Afya ya Wanawake (FORWARD) pamoja na Shirika la Utafiti juu ya Kupunguza Umasikini (REPOA).

Baada ya utafiti huo kukamilika, iliandaliwa ripoti ambayo ilizinduliwa mnamo Machi, 2 mwaka huu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ripoti inayojulikana kama Ripoti ya Utafiti wa Visababishi na Madhara ya Ndoa za Utotoni Nchini Tanzania.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa umasikini ndio sababu kubwa inayopelekea kuwepo kwa ndoa za utotoni.
Baadhi ya mikoa ambayo wananchi walihojiwa wakati wa utafiti wamekubali kwa nguvu zote kuwa fedha zinazolipwa kwa ajili ya mahari ndizo zinazowasababisha kuwaoza watoto wao wakiwa bado wadogo.

Utafiti huo unaonesha mkoa wa Mara wananchi asilimia 59 wanakubalina na majibu ya utafiti huo ambapo mkoa wa Dar es Salaam asilimia 56, mkoa wa Dodoma asilimia 53, mkoa wa Lindi asilimia 52 na mkoa wa Tabora asilimia 51.

Sababu nyingine ya ndoa za utotoni ni mtazamo wa tamaduni, mila na desturi baina ya jamii mbalimbali kuhusu miaka ya mtoto wa kike anayetakiwa kuolewa, unyago, ukeketaji pamoja na ngoma za asili zinazopelekea watoto kuozwa mapema.

Tafiti hizo zinaonyesha kwamba maeneo ya vijijini asilimia 18 ya wanawake wamekeketwa wakati Mijini ni asilimia 7 na Mikoa inayoongoza ni Manyara asilimia 81, Dodoma asilimia 68, Arusha asilimia 55, Singida asilimia 43 na Mara asilimia 38.

Aidha, asilimia 24 ya waliohojiwa mkoani Shinyanga na asilimia 20 ya mkoani Tabora wamesema mikoa hiyo ina kiwango kikubwa cha ndoa za watoto walio na umri chini ya miaka 18.

Utafiti huo pia umegundua kuwa ukosefu wa elimu unapelekea wasichana kuingia kwenye ndoa wakiwa bado wadogo kiumri hii inatokana na kushindwa kuendelea na masomo baada ya kumaliza elimu ya msingi.

Kutokana na utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Plan International- Tanzania, Jorgen Haldorsen anasema “Matokeo ya utafiti huo yanawapa mwongozo wa kujua sehemu zilizoathirika zaidi ili kuweka nguvu za kutosha na kufahamu namna mbalimbali za kutumia kuwafikia waathirika hao”.

Akizindua ripoti hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema kuwa anapozindua ripoti hiyo ni dhahiri anapinga kwa vitendo ndoa na mimba za utotoni kwani ni changamoto kwa maendeleo ya Tanzania.

“Tunataka Tanzania kuwa nchi ya viwanda, lakini hatutaweza kuwa na nchi yenye viwanda wakati watoto 36 katika kila watoto 100 nchini wanaolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18 na watoto 27 wa kitanzania wanapata mimba kabla ya umri huo, hili ni tatizo kubwa ambalo athari zake zitaonekana baadae”anasema Waziri Ummy.

Katika kuhakikisha ndoa hizo zinakoma, Waziri Ummy ameanza kutumia marekebisho ya Sheria ya Elimu yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo June 2016 ambayo yanakataza mtu yoyote kumuoa mtoto wa shule ya Msingi au Sekondari kwani ni kosa la jinai lenye adhabu ya miaka 30 jela.

Pia, Waziri Ummy amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kila Halmashauri kupita nyumba kwa nyumba kuwaibua wazazi wanaofanya vitendo hivyo na kuwasilisha taarifa hizo sehemu husika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sheria hiyo.

Waziri Ummy ameyaahidi mashirika hayo ya kutetea haki za watoto kuendelea kushirikiana nao katika kuwapa semina wazazi juu ya athari za ndoa za utotoni, kuwapa watoto elimu ya afya ya uzazi pamoja na kuboresha mazingira ya shule ili kuwawezesha wasichana kupata hamasa ya kwenda shule.

Kwa upande wa viongozi wa dini Mchungaji Cistus Mallya pamoja na Sheikh Swedi Twaibu wanasema mtoto lazima apate malezi mazuri kutoka kwa wazazi ili aweze kufahamu mabaya na mazuri na aweze kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo vya kudanganywa na kuingia katika mapenzi wakiwa na umri mdogo.

Viongozi hao wamemuomba Waziri Ummy kuangalia utaratibu wa kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili nao baadae waje kuwa wanawake wanaoweza kuleta maendeleo katika taifa lao.

Akiwakilisha vijana wa kike, Catherine Kapilima amesema ndoa za utotoni uhathiri afya, elimu na maendeleo ya mtoto wa kike.

Aidha, Catherine amesema kuwa wazazi kupewa elimu pekee haitoshi kwani kuna wengine ambao sio waelewa, hivyo ni jukumu la Serikali kuweka nyumba ambazo ni salama kwa ajili ya kuwapokea na kuwapatia huduma muhimu watoto wa kike wanaokimbia kutoka kwa wazazi wasiokuwa waelewa.

Ni wakati muafaka sasa Wadau wote wa Maendeleo nchini kwenda zaidi Vijijini kuwasaidia wanawake na wasichana waliopo huko kwani ndio maeneo yenye waathirika wengi wa ndoa na mimba za utotoni ikilinganishwa na mijini.

Ikiwa Dunia inakarabia kuadhimisha siku ya wanawake duniani mnamo Machi, 8 mwaka huu, Serikali, wadau pamoja na wananchi waungane kwa pamoja kuzuia ndoa za utotoni ili kuandaa wanawake imara katika miaka ijayo.

Tunaamini kuwa watoto wa kike wa sasa ndio wanawake wa kesho hivyo ni vema kuwaandaa kuwa wanawake bora wenye kuweza kujitegemea na watakaoweza kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi nchini.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Post a Comment